Na FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM
KATIKA harakati zinazoendelea hivi sasa, kuelekea Tanzania ya viwanda, wajasiriamali wanaojishughulisha na uzalishaji mali nchini wamekuwa chachu ya mafanikio katika serikali kutokana na kuonyesha uwezo, jitihada na ujuzi katika kukuza uchumi wa nchi.
Wajasiriamali wengi hufanya shughuli zao za uzalishaji wa aina mbalimbali ili kuiweka nchi katika hali nzuri ya maendeleo kama nchi nyingine, ili kukuza biashara kuwa ya kimataifa zaidi.
Kwa muda mrefu sasa tumeona taasisi na mashirika mbalimbali nchini yamekuwa yakijitokeza katika kukuza biashara na uzalishaji wa viwanda mbadala.
Lakini kwa sasa imekuwa ni hali ya kawaida kuanzishwa kwa taasisi na mashirika, vilevile ongezeko la wajasiriamali kuzidi kushika kasi katika biashara ya mbali hadi kuvuka mipaka kibiashara kufikia Afrika Mashariki nzima.
Wajasiriamali wadogo waliounda kikundi kinachojulikana kama “Nohindu Company Limited”, kilichoanzishwa mwaka 2015 chini ya Shule ya St Anthony’s jijini Dar es Salaam, chini ya mwenyekiti wa kikundi Richard Caesar, kinaendelea vizuri.
Lengo kuu la kuanzishwa kwa taasisi hiyo yenye wajasiriamali wadogo ni kupanua njia za ajira kwa vijana kwa kutokutegemea elimu ya darasani pekee na hatimaye kuwa na elimu mbadala ambayo itakuwa ni chachu kwa jamii.
Caesar anasema kuwa, taasisi ya Nohindu Company Limited ilianzishwa ikiwa na wanachama 13, ambao hadi sasa ndio wanaofanya maendeleo ya ujasiriamali.
Anaongeza kusema kuwa, hadi sasa kiwango cha biashara kama taasisi walipofikia ni hatua nzuri ambayo inawafanya wajulikane zaidi kuwa wajasiriamali wadogo wanaochipukia katika biashara.
“Bidhaa zinazozalishwa na taasisi hiyo ni mchele, kuku wa kienyeji, maziwa freshi yanayotoka katika Mkoa wa Tanga na maharage.
Vilevile taasisi hiyo inazalisha mazao kama vile mbogamboga mbalimbali za majani kama mchicha na majani ya maboga,” anasema Caesar.
Anasema vilevile bidhaa hizo zinauzwa kwa reja reja katika duka linalomilikiwa na taasisi hiyo na kuuza katika njia ya mtandao.
“Kutokana na biashara hiyo ilivyokuwa, kama taasisi inawakaribisha wateja wote na kwa yeyote atakayehitaji anaweza kuletewa hadi mahali pale alipo, kwani kama taasisi inamjali na kumudu haja ya mteja popote alipo,” anasema Caesar.
Anaongeza kuwa, katika hatua waliyofikia hawawezi kuishia hapo, kwani hapo ni mwanzo tu na wanatarajia kuiendeleza zaidi.
Biashara hiyo ya bidhaa mbalimbali ambayo hufanywa kwa njia ya mtandao ni kuwawezesha zaidi vijana wengine ili waweze kujiunga na taasisi hiyo na kuwa wajasiriamali wakubwa zaidi.
Matarajio ya taasisi hiyo ni kuwa na Kampuni kubwa zaidi hapo baadaye, kutokana na juhudi za ujasiriamali zinazofanywa na vijana hao, wanatarajia kukua na kufikia ukubwa wa kampuni kama alivyo Bakhressa na kuhakikisha kuwa kila mmoja wao anakuwa mmiliki wa sehemu ya kampuni kwa kuwa na hisa.
Anasema hadi kufikia mwaka 2017 tangu chama kianzishwe, kina zaidi ya Sh milioni moja kutoka mtaji wa Sh 2,000, kwa hiyo ni mafanikio makubwa yaliyopatikana, ndani ya mwaka mmoja pekee.
Fedha za mtaji zilitokana na michango mbalimbali iliyotokana na wanachama hao, ‘wanafunzi’ ambapo mwanzo ilikuwa ni kwa lengo la kusaidiana katika shida mbalimbali.
Lakini kutokana na kuongezeka kwa kipato siku hadi siku na kufikia kuwa taasisi ni mafanikio makubwa yaliyofanywa na kikundi hicho cha vijana 13 ambao waliona ni vyema kuwa wajasiriamali ambao wanazalisha bidhaa za soko.
Anasema licha ya kuwa wajasiriamali, lakini pia huwa ni waungwana wema ambao mara nyingi hutenga muda kwa ajili ya kuwatembelea watoto yatima na waishio katika mazingira hatarishi katika vituo mbalimbali nchini.
“Hadi sasa kama taasisi imetembelea zaidi ya vituo 4 vya watoto yatima, ikiwamo kuwajulia hali zao na kuwapatia misaada mbalimbali ya kijamii ambayo itawasaidia katika matumizi mbalimbali pindi wawapo katika kituo.
“Taasisi ya Nohindu inawaasa vijana na taasisi nyingine kuiga na kuwa mfano kutoka kwao, ingawa bado ni kampuni changa lakini ina malengo stahiki, ili kutokuwa tegemezi sharti ni kujishughulisha,” anasema Caesar.
Anasema kama taasisi inachipukia lazima kuwe na vikwazo na changamoto mbalimbali, zikiwamo changamoto ya ukosefu wa masoko ya kusambazia bidhaa, kuwapo kwa dharau kutoka kwa wateja, mtaji mdogo usiotosha kufikia malengo.
Vilevile kama taasisi inayofanya biashara katika mtandao, inahitaji kuwa na usafiri wa haraka ili kuweza kumfikia mteja pale anapohitaji bidhaa kwa haraka.
Pia Caesar anaongeza kuwa, changamoto nyingine inayowakabili pindi wawapo katika soko la biashara, yaani mtandaoni kuna baadhi ya watu huwabeza na kuwadharau, hata wengine huwavunja moyo wa kutokuendelea kufanya biashara ili tu wasiweze kufikia malengo stahiki waliyojiwekea katika taasisi hiyo.
“Kama taasisi tunaiomba jamii iweze kutuunga mkono ili kufikia malengo stahiki tunayotarajia katika shughuli ya ujasiriamali,” anasema Caesar.
Vilevile inatoa ombi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweza kutambua uwepo wao na mchango wao wa hali na mali ili waweze kufikia malengo stahiki wanayotarajia, na wanahitaji kuungwa mkono.
Pia wanaomba serikali itambue mchango utolewao na wajasiriamali wote wadogo, ukizingatia ni taasisi ya wajasiriamali wadogo waliothubutu kufanya biashara ya mtandaoni na wakaweza, lengo ni kutanua soko la ajira kwa vijana ili waweze kujiajiri wenyewe.