Na Dixon Busagaga-Kilimanjaro
ZAIDI ya Mawakala 50 wa Benki ya CRDB katika mkoa wa Kilimanjaro wakiwemo wanaofanya shughuli zao katika mpaka wa nchi jirani ya Kenya wamepewa mafunzo juu ya tahadhari na kujiepusha na matukio ya utakatishaji fedha .
Mafunzo hayo yaliyotolewa na maofisa kutoka makao makuu na Kanda ya Kaskazini.
Miongoni mwa mawakala waliopatiwa mafunzo hayo ni kutoka maeneo ya Mwanga, Himo ,Marangu, Rombo Mkuu, Tarakea na Holili ikiwa ni muendelezo wa mafunzo yanayofanyika nchi nzima .
Akifungua mafunzo hayo katika Hoteli ya African Flower iliyopo mji mdogo wa Himo, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dk Anna Mghwira alisema ni rahisi kwa wahalifu kujaribu kuwatumia .
“Kupitia mafunzo haya mazuri mtaweza kupewa elimu ya kumtambua mteja wako na kumuhudumia ipasavyo na kukuwezesha kulinda na kukuza mtaji wako uweze kufanya kazi vyema zaidi.” Alisema Dk Mghwira .
Alisema uwakala wa kibenki umefungua fursa nyingi na kuwezesha kukua kwa uchumi na kwamba serikali inajivunia uwepo wa mawakala kwa kufungua milango ya urahisi wa kukusanya kodi kwa kuwezesha wananchi kulipia kodi popote.
“Wakala wa CRDB ni moja ya njia zinazoongoza kupendwa na wananchi kulipia kodi ambapo naambiwa zaidi ya miamala milioni 8 yenye thamani zaidi ya Bil 300 zilikusanywa kupitia wakala wa CRDB kwa mwaka Jana tu.”alisema Dk Mghwira
“Na kwa nusu ya mwaka huu tayari mmesaidia serikali kukusanya zaidi ya Bil 350…hii ni dhihirisho kwamba uwakala wa CRDB ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya Taifa kwa ujumla.”aliongeza Dk Mghwira .
Naye Meneja wa CRDB Kanda ya Kaskazini ,Chiku Issa alisema CRDB ndio benki ya kwanza kuanzisha huduma za mawakala wa benki ambazo ilianzisha mwaka 2013 na kwamba kwa sasa ina mawakala zaidi ya 16,000 waliotapakaa Tanzania nzima.
“Moja ya lengo la kuandaa semina hii ilikuwa kuwashukuru mawakala hao katika kutambua mchango wao katika kukubali kushirikiana na benki ya CRDB katika kupeleka huduma karibu na wateja lakini pia kuwajumuisha wananchi kwenye huduma za kifedha (financial inclusion)”alisema Chiku
Alisema mawakala wa CRDB wamesaidia kuongeza huduma za kibenki kwa kuongeza muda wa wateja kufanya miamala ambapo baadhi ya mawakala wanatoa huduma kwa masaa 24.