Na ASHA BANI
*Dk. Mpango asifu mabadiliko, ataka taasisi nyingine ziige
ILI kufikia Tanzania ya viwanda, kunahitajika mambo mbalimbali yatakayofanikisha kufikia lengo hilo.
Lakini taasisi za fedha nazo zina mchango mkubwa kutokana na kuwa kichocheo katika uendelezaji, ukuzaji wa masoko, wajasiriamali na hatimaye kuwa na uchumi wa viwanda nchini.
Hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa jina na nembo mpya ya Benki ya Posta Tanzania, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alielezea umuhimu wa mabenki na hasa Benki ya Posta katika kusaidia kukuza uchumi .
Dk. Mpango anasema sekta ya mabenki ndio inayokua kuliko sekta nyingine yoyote.
Anasema kitendo cha uongozi wa benki kubuni njia mbalimbali hasa ya kubadilisha nembo na hata kuongeza idadi ya matawi na kupanua wigo mpana wa matawi, kunachangia kufanya mabadiliko katika sekta ya fedha.
Aliyataja mabadiliko hayo kuwa ni pamoja na kusaidia kuleta viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa.
“Tena Benki ya Posta ipo vizuri kutokana na kusaidia akina mama waliojiunga katika vikundi na kupata mikopo ya kuendeleza ujasiriamali wao,” anasema.
Sambamba na hayo, aliisifu Bodi ya Benki ya Posta kwa kufanya kazi nzuri hasa ya kuwasaidia wastaafu na vikundi mbalimbali vilivyopo vijijini.
Historia
Benki ya Posta Tanzania ni moja katika ya taasisi kongwe za fedha nchini ambayo imepita katika mawimbi mazito hadi kufikia ilipo sasa.
Hatua hiyo inatokana na namna biashara ya benki inavyohitaji mtaji mkubwa sana ambao ilisababisha benki hiyo kuwa omba omba ili kukidhi mahitaji yake kibiashara.
Tangu kuanzishwa kwake, TPB haijawahi kuwa na mtaji wa kujitosheleza na kukidhi matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha na wanahisa wake hawajaweza kuongeza mtaji wa kutosha kwenye benki yao.
Benki Kuu ya Tanzania katika kanuni zake zilizofanyiwa marekebisho mwaka 2014, imeongeza hitaji la mtaji kwa benki zote nchini ambapo uwiano wa mtaji na mali hatarishi (capital to risk assets) umeongezwa hadi asilimia 14.5 kutoka uwiano wa awali wa asilimia 12.
Benki zote nchini zinatakiwa kufikia uwiano huu wa mtaji ifikapo Agosti mwaka huu. Hadi kufikia Desemba mwaka jana, uwiano wa Benki ya Posta Tanzania ulikuwa asilimia 12.94, ikiwa ni chini ya matakwa ya sheria.
Mahitaji haya ya mtaji ni makubwa sana na hivyo italazimu benki zote nchini kuongeza mitaji yao hasa zile ambazo mitaji yake iko chini kama TPB.
Kutokana na hali hiyo, benki hiyo imeanza safari ya maandalizi ya kuuza hisa zake katika soko la hisa na mitaji ili kuongeza mtaji wake.
Hatua hizi zinatarajiwa kukamilika ifikapo Juni mwaka huu.
Yapo maombi mengi ikiwemo kuhitajika msaada wa Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, kuhakikisha anasaidia harakati hizo za kuikwamua benki kutokana na tatizo kubwa la mtaji.
Mwaka 2011, uongozi wa juu wa benki hiyo ulibadilishwa kwa kumleta Ofisa Mtendaji Mkuu mpya, Sabasaba Moshingi ambaye amekuwa akihaha kuiokoa benki hiyo ili iweze kuwa na ufanisi wa kutosha na kuwa na ushindani wenye faida kubwa kwa wateja wake.
Tangu wakati huo mwaka 2011 hadi sasa, yapo mafanikio kadhaa yaliyofikiwa, ikiwemo idadi ya matawi makubwa na madogo yameongezeka kutoka 32 mwaka 2011 hadi kufikia 60 mwaka 2016.
Matawi mengi yalikuwa yamechakaa sana na sasa karibu yote yamekarabatiwa, jambo ambalo ni zuri na lenye kuonyesha taswira chanya kwa benki hiyo.
Si hilo tu hata mikopo iliyoanzishwa katikati ya mwaka 2014 imefikia thamani ya Sh bilioni 4.5 ambapo wateja hudhaminiana wao kwa wao bila kuweka dhamana.
Si hilo tu benki hiyo imekuwa ikitoa mafunzo ya utunzaji wa kumbukumbu za fedha na jinsi ya kufanya biashara zenye tija.
Binafsi nafurahishwa na maendeleo makubwa kuiona Benki ya Posta Tanzania ikipiga hatua, ambapo kutokana na hali hiyo ninajua ipo mikopo ilianzishwa Desemba mwaka 2015, ikiwemo ile iliyotolewa kwa ushirikiano na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Thamani ya mikopo hiyo kwa sasa ni Sh milioni 701, ambayo hudhaminiwa na NEEC kwa asilimia 50 na muda wa marejesho huwa kati ya miezi 4 – 12.
Siku zote Benki ya TPB huamini katika kutoa huduma za kijamii ili kuwapunguzia wananchi matatizo wanayokabiliana nayo.
Benki ya Posta Tanzania ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 11 ya mwaka 1991 (kama ilivyofanyiwa mabadiliko mwaka 1992).
TPB ndiyo benki pekee ambayo ilikuwa imebaki ikiwa imesajiliwa chini ya sheria ya Bunge kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha (BAFIA, 2006).
Jitihada za kuisajili benki hiyo chini ya sheria ya makampuni zilianza mwaka 2007 na safari yake sasa imefanikiwa.
Ilipofika Juni 2015, Bunge lilipitisha sheria ya kuifuta sheria iliyoianzisha benki hiyo na kuruhusu isajiliwe chini ya sheria ya makampuni na wanahisa wa benki kwa kauli moja, hapo Machi 29, mwaka jana waliidhinisha jina jipya na hivyo kuruhusu benki hiyo isajiliwe chini ya sheria ya makampuni.
Kwa hakika mabadiliko haya ya kwenda Soko la Hisa la Dar es Salaam na kuja na mwonekano mpya wa nembo ya Benki ya Posta Tanzania, naiona ni safari ya mafanikio kuelekea kwenye neema zaidi.