HABARI ZOTE Na WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi, amesema kanuni zinamruhusu kugombea tena uongozi katika kamati hiyo.
Bayi ametoa kauli hiyo kutokana na baadhi ya wadau wa michezo nchini kudai kuwa anang’ang’ania madaraka, kwani ameiongoza kamati hiyo kwa muda mrefu.
Katibu huyo bado hajaweka wazi kama atagombea kutetea nafasi yake katika uchaguzi mkuu ujao ambao umepangwa kufanyika Desemba 10, mwaka huu mjini Dodoma.
Alisema akiamua atagombea kwani kanuni za Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC), zinaeleza kuwa mwisho wa ukomo wa mgombea ni miaka 70 ambayo bado hajaifikisha.
“Umri wangu unaniruhusu kugombea tena kama nitataka kufanya hivyo kwa mujibu wa kanuni za IOC, lakini ninaamini kabla sijafika huko nitawapa nafasi wengine,” alisema.
Akizungumzia uchaguzi ujao wa TOC, mwanariadha huyo wa zamani aliwataka wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali ili waweze kutoa michango yao kwenye kamati hiyo.
Fomu za kuwania uongozi zitaanza kutolewa kesho katika ofisi za TOC upande wa Tanzania Bara na visiwani, ambapo gharama kwa nafasi ya Rais, Makamu wake, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina Mkuu na msaidizi wake ni Sh 200,000 na wajumbe ni Sh 150,000.
Sifa za mgombea ni kuwa raia wa Tanzania anayekubalika kwenye jamii na mwenye uzoefu katika uongozi wa michezo kitaifa na kimataifa.