Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
BARAZA la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) limemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick kuyataja hadharani majina ya wakazi wa mabondeni waliogawiwa viwanja Mabwepande.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mwenezi wa Bavicha, Edward Simbei, alisema wanamtaka Sadick kutaja majina hayo jamii ijue idadi ya wakazi waliogawiwa viwanja na serikali kwa ajili ya kuhamia Mabwepande.
“Kuna minong’ono kwamba waliopewa maeneo Mabwepande si wale waliostahili na mkuu wa mkoa anahusika katika hilo ingawa mwenyewe amejitokeza na kukanusha taarifa hizo.
“Serikali imebomoa makazi ya watu waishio mabondeni kule Mkwajuni na Jangawani, Bavicha tunaunga mkono jambo hilo lakini asilimia kubwa wanasema hawakugawiwa viwanja huko Mabwepande,” alisema.
Alisema hali hiyo imesababisha wakazi hao kubakia mabondeni licha ya kubomolewa nyumba zao jambo ambalo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
“Serikali ilipaswa kufanya tathmini kwanza kujua wangapi walikuwa ni wamiliki wa nyumba zile na wangapi walipanga kabla ya kuvunja na kuwapa muda wa kuondoka wenyewe kabla ya kuwabomolea ambako hadi sasa takriban watu 30 wamefariki dunia akiwamo mtoto wa miezi minne,” alisema.
Alisema hatua hiyo ya kubomoa nyumba za mabondeni ni ya unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu ambayo Bavicha wanaipinga.