Na Beatrice Kaiza, Mtanzania Digital
Waziri wa zamani wa Fedha katika Serikali ya wamu ya tatu, Basil Mramba(81) amefariki dunia.Kwa mujibu wa mtoto wake, Godfrey Mramba, baba yake amekutwa na umauti leo asubuhi wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Regency.
“Mzee amefariki mapema leo Agosti 17, 2021, ameugua pale Regency Medical Centre muda wa wiki mbili, amepata maradhi ya Covid-19 tumempoteza leo, tunamshukuru Mungu kwa maisha yake na tutayasherehekea,” amesema Godfrey.
Kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini kimetokea leo kwa ugonjwa wa UVIKO-19.
Aidha, Godfrey ameweka wazi kuwa, kutokana na janga la virusi vya Corona (Uviko-19) msiba huo utahusisha watu wa familia pekee ili kuepuka mkusanyiko.