22.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

NMB Marathon 2021 yazinduliwa, mapato kutibu wagonjwa Fistula CCBRT

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI ya NMB, imesaini makubaliano ya ushirikiano na Hospitali ya CCBRT, yanayolenga kukusanya kiasi cha Sh Bilioni 1 (katika kipindi cha miaka minne) za matibabu ya Fistula kwa kina mama wasio na uwezo, kupitia Mbio za Hisani za NMB Marathon, zitakazofanyika kwa mara ya kwanza Septemba 18, 2021 jijini Dar es Salaam.

Kupitia NMB Marathon, ambazo mwaka huu zitafanyika chini ya kaulimbiu ya: ‘Mwendo wa Upendo,’ Benki ya NMB na CCBRT wanatarajia kukusanya zaidi ya Sh.\ milioni 250 (kila mwaka), ambazo zitasaidia matibabu ya wagonjwa 60 wa Fistula, miongoni mwa mamia ya kina mama wanaoteseka kwa maradhi hayo.

Akizungumza wakati wa utilianaji saini wa makubaliano na uzinduzi wa mbio hizo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema kuna kila dalili za kufikia lengo la makusanyo hayo, hasa kutokana na uungwaji mkono waliopata kutoka Kampuni za Bima za Sanlam na UAP, ambazo zimechangia Sh. Milioni 100 (sawa na Sh mil 50 kila moja).

“Lengo ni kukusanya Sh. Bilioni 1, kiasi ambacho ni sawa na Sh mil 250 kila mwaka. Watanzania wajitokeze kuungana nasi katika mbio hizi, ili kuokoa maisha ya wamama wanaoteseka na maradhi ya Fistula. Tuna mwezi mzima wa kujisajili na naamini tunaweza kufikia lengo kwa ushirikiano huu,” alisema Zaipuna.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi, alisema taasisi yake inajisikia faraja kubwa kufanikisha utilianaji saini wa makubaliano hayo, sambamba na uzinduzi wa NMB Marathon 2021, huku akieleza kuwa mashindano hayo yana maana kubwa kwa maelfu ya kina mama wa Kitanzania.

“CCBRT ni wabobevu wa matibabu ya Fistula nchini, na tafiti zetu za awali zilionesha ukubwa wa tatizo miongoni mwa kinamama, lakini gharama kubwa za matibabu unakwamisha wengi wao kupata tiba za maradhi haya. 

“Ndio maana tunachukua nafasi hii kuwapongeza NMB kwa uamuzi wao wa dhati wa kuwabeba wamama wa Kitanzania takribani 60 watakaolipiwa Sh mil 250 kila mwaka katika kipindi cha miaka minne. Kila Mtanzania anapaswa kuunga mkono jitihada hizi chanya kwa afya za kina mama,” alisema Msangi.

NMB Marathon zitakuwa na kategori tatu za mbio za kilomita 21 (nusu marathon), kilomita 10 na kilomita 5, ambako washindi wa kwanza hadi wa 10 watapata medali na fedha taslimu.

Kwa mujibu wa Mratibu wa NMB Marathon 2021, David Marealle, ada ya kujisajili kushiriki mnio hizo ni Sh. 30,000 kwa kilomita 21 na Sh 20,000 kwa mbio za kilomita 10 na kilomita 5.

Marealle aliongeza kuwa, washindi wa mbio za kilomita 21 wanaume na wanawake watajinyakulia Medali ya Dhahabu na fedha taslimu Sh 1,400,000, huku washindi wa pili wakitarajiwa kutwaa Medali za Fedha na Sh. 1,100,000, wakati washindi wa tatu wakitengewa Sh 700,000 na Medali za Shaba.

Zawadi za washindi wa kilomita 10 wanawake na wanaume ni: kinara medali ya dhahabu na Sh 700,000, washindi wa pili medali za fedha na Sh. 500,000, huku washindi wa tatu wakitarajiwa kubeba medali za Shaba na Sh 300. 

Katika mbio za kilomita 5, washindi upande wa wanawake na wanaume watajipoza na Medali za dhahabu na Sh. 250,000, washindi wa pili medali za fedha na Sh 150,000, huku washindi wa tatu wakiambulia medali za shaba na Sh 100,000 taslimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles