23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Bashungwa kuendeleza alipoishia Dk. Mwakyembe

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema kuwa mambo yote mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake Dk.Harrison Mwakyembe katika sekta anazozisimamia atayaendeleza ili matarajio ya kuundwa kwa kwa Wizara hiyo yafikiwe.

Bashungwa ameyasema hayo leo Ijumaa Desemba 11, wakati akipokea Ofisi kutoka kwa Waziri mstaafu Dk. Harrison Mwakyembe ambapo ameeleza kuwa ataendelea kushauriana na naye katika masuala mbalimbali ya wizara hiyo kutokana na uzoefu aliyonao, huku akisitiza kuwa mahusiano mazuri na watu katika maeneo mbalimbali ya kazi na jamii ni muhimu kwa sababu manufaa mengi.

“Tulishirikiana na wewe katika kuhamisha Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA) kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kuja wizara hii,nimatumaini yangu tutaendelea kushirikiana katika sekta zote za wizara hii”, amesema Bashungwa.

Akiendelea kuzungumza Waziri Bashungwa alisema kuwa tayari ameaviagiza Vyama vya Michezo kuwasilisha mpango mkakati wa namna ya kuendesha michezo nchini, huku akisisitiza suala la Makampuni ya Michezo ya Kubahatisha kuchangia katika ustawi wa Timu za Taifa.

Aidha, Bashungwa ameiagiza Bodi ya Filamu Tanzania kuona namna ya kuanzisha mfumo ambao utatumika kuuza kazi za filamu kwa mfumo wa kidigitali kama ilivyo ‘Netflix’ kwani itasaidia wasanii kusambaza kazi zao kwa urahisi na pia kuchangia katika pato la taifa ambapo alisisitiza kuwa “Msanii kiwanda chake ni kichwa chake,”.

Naye, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Abdallah Ulega amesema jambo la kuwa na Shule za Michezo (Sports Academy) ni jambo la msingi ambalo uongozi wao utalifanyia kazi na kuweka mkazo katika michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA ili timu ya taifa itokane na vijana hao.

“Tumejipanga kuhakikisha tunalinda Utamaduni wa Taifa Letu, vijana tunaowajibu wa kuhakikisha tunu za nchi pamoja na maadili ya nchi yetu tunayalinda, na katika sekta ya Sanaa tunatambua Sanaa ni ajira hivyo tutasaidia kuikuza,” amesema Ulega.

Awali, akiwakaribisha viongozi hao Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali, Hassan Abbasi alisema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Dk. Mwakyembe kumekuwepo na mafanikio mengi ikiwemo ongezeko la Bajeti pamoja na utatuzi wa changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika wizara hiyo.

Katika ufafanuzi wake Dk. Abbasi alisistiza kuwa Dk.Mwakyembe alisimamia vyema sekta ya Habari ambapo alihakikisha Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016, inafuatwa pamoja na Kanuni zake ambapo alisisitiza kuwa sekta ya habari ni taaluma na vyombo vya habari vina haki na wajibu.

“Katika uongozi wako Dk. Mwakyembe ulifanya mambo mengi, ulitatua mgogogo kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Kampuni ya Startimes ambao uliyokuwa umedumu kwa muda mrefu, umeongoza kuanzishwa kwa Tanzania Safari Chaneli, umefanya maboresho makubwa katika shirika hilo ikiwemo kuanzishwa kwa kipindi cha Aridhio, umesimamia sekta ya michezo kwa kutunga Kanuni za Baraza la Michezo la Taifa pamoja na kuunda Kamati ya Kusimamia Haki za Wasanii”,alisema Dk.Abbasi.

Kwa upande Waziri huyo aliyemaliza muda wake Dk.Harrison Mwakyembe amewashauri viongozi hao kutambua umuhimu wa kuundwa kwa Wizara hiyo tangu enzi za Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere ambapo lengo lilikuwa ni kulinda historia ya nchi.

Dk. Mwakyembe amesema kuwa wizara hiyo ina Sekta ya Utamaduni ambayo ni kiini na roho ya taifa kwa kuwa inaeleza mambo mbalimbali ya taifa ikiwemo lugha ya Kiswahili, umuhimu wa Wimbo wa Taifa ambapo ni lazima kuimbwa shuleni kila siku na kwenye  shughuli mbalimbali za kitaifa ambapo Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 imeeleza kuwa ni  jambo hilo ni la lazima.

Vilevile Dk.Mwakyembe amesema kuwa sekta ya habari inatambulika katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, wananchi wana haki ya kupata taarifa na habari sahihi na sekta ya michezo na Sanaa zinatoa fursa kwa vijana ikiwemo kujiajiri hivyo ni muhimu zikaendelea kuendelezwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles