Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa, ameliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lishirikiane na Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania,(CHAMUDATA) kumpeleka hospitali mwanamuziki mkongwe, Hussein Abdallah ‘Stima’ mwenye umri wa miaka 85 anayesumbuliwa na maradhi ya moyo na presha tangu mwaka 2020 ili aweze kupata matibabu.
Bashungwa ametoa agizo hilo leo Novemba 30, 2021, alipomtembelea Stima nyumbani kwake Buguruni kwa Mnyamani jijini Dar es Salaam kumjulia hali.
“Fanyeni taratibu zote zinazohitajika haraka ili mzee wetu apatiwe matibabu, hili linawezekana,” amesisitiza Bashungwa.
Aidha, Stima ameishukuru Serikali na kutoa wito kwa wasanii kuimba nyimbo zinazohamasisha maendeleo ya Taifa na uzalendo kwa nchi yetu.
Stima ni miongoni mwa wanamuziki nguli nchini anayejulikana kwa umaridadi wake wa kupuliza saxophone unaowakosha watu wengi ikiwa ni pamoja na hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Enzi za ujana wake amefanya kazi katika bendi mbalimbali ikiwa Cuban Marimba, JWTZ Mwenge Jazz, Vijana Jazz, S.A. Rhumba na Washirika Njatanjata.