BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata), limezidi kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya matamasha ya Krismasi na Pasaka, ambayo yanaonekana kuchangia maendeleo ya muziki wa injili Tanzania.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, matamasha ya Msama yanachangia maendeleo ya muziki wa injili ambayo ndiyo njia ya kufanikisha ujumbe wa neno la Mungu hasa kwa matukio mbalimbali.
Mngereza alitoa pongezi kwa Msama hasa kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka ambapo inabidi tumrudie Mungu ili tuanze mwaka mpya tukiwa wapya.
Katibu Mtendaji huyo alisema inabidi tumrudie na kumkimbilia Mungu baada ya kupita kwenye uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu, hali ambayo nchi jirani hawana.
Aidha, Mngereza alisema waimbaji wa muziki wa injili wanatakiwa kujifunza zaidi kutoka kwa waimbaji wa nje ambao wamepiga hatua zaidi katika muziki huo.
“Tamasha la Krismasi ni letu sote, tutoe sapoti kwa Msama ambaye anafanikisha kazi za waimbaji wa muziki wa injili ambao eneo lingine wanatuunganisha na Mungu kwa njia ya uimbaji,” alisema Mngereza.