ZAMDA BIWI NA IDDY ABDALLAH, (RCT)
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limepanga kutoa tuzo tano kwa wasanii waliochangia jamii na waliotumia maisha yao yote katika maendeleo ya sanaa kwa ujumla nchini.
Tuzo hizo zitakazotolewa katika maadhimisho ya siku ya msanii yatakayofanyika Desemba 12, katika ukumbi wa Blue Pearl uliopo jijini Dar es Salaam, yatakuwa na kauli mbiu ya ‘Nguvu ya Sanaa’.
Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Masoko, Nsao Vivian, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kumtambulisha msanii, kazi zake pamoja na mchango wake katika jamii.
Vivian aliongeza kwamba siku hiyo inatarajiwa kuwa na matukio mbalimbali, ikiwemo maonyesho ya kazi za sanaa za ufundi katika makumbusho na nyumba ya utamaduni.
Naye Rais wa sanaa za maonyesho Tanzania, Agnes Lupamba, alisema sanaa ina nguvu kubwa katika kubadilisha fikra kwa jamii, ndiyo maana wameandaa mjadala kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili sanaa kwa ujumla.