UONGOZI wa klabu ya Rangers jana umemsimamisha kwa wiki tatu kiungo wa timu hiyo, Joey Barton, baada ya kukutwa na hatia ya kupigana na mchezaji mwenzake, Andy Halliday.
Uamuzi huo ulifanyika ikiwa ni siku sita baada ya nyota huyo kurudishwa kwao kutokana na kutuhumiwa kufanya kitendo hicho.
Barton mwenye umri wa miaka 34, alikiri kufanya kitendo hicho katika kikao kilichofanyika jana klabuni hapo.
Kwa mujibu wa Meneja wa klabu hiyo, Mark Warburton, klabu hiyo inahitaji muda na nafasi ya kujadili tatizo hilo.
“Mmoja kati ya Barton au Halliday, anatakiwa kuandaa maelezo kuhusu tukio hilo,” alisema Warburton.
Inafahamika kuwa ugomvi kati ya wachezaji hao ulitokea wiki iliyopita wakati timu yao ilipofungwa mabao 5-1 dhidi ya wapinzani wao Celtic.
Baada ya kutokea kitendo hicho, klabu iliwataka kuondoka na kurejea jana ambapo uongozi wa klabu hiyo ulifanya uamuzi.
Katika utetezi wake, Barton alikiri kukosea na aliomba msamaha kwa kitendo chake cha kumvamia mchezaji mwenzake.
“Miongoni mwa vitu nilivyofanya havikuwa sahihi, sikutakiwa kufanya nilichofanya, naomba nisamehewe.
“Kuomba msamaha haimaanishi kuwa kila siku nitakuwa na makosa na mtu mwengine atakuwa sahihi, maana yake ni kuongeza uhusiano zaidi kwa wengine,” alisema Barton.
Kosa jingine alilolifanya nyota huyo ni kuzungumza katika vyombo vya habari bila kupewa ruhusa na klabu hiyo.