Sakata la Escrow laielemea Tanesco

0
786
Profesa Sospeter Muhongo.
Profesa Sospeter Muhongo.
Profesa Sospeter Muhongo.

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

UAMUZI wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID), kulitaka Shirila la Umeme Tanzania (Tanesco) kuilipa Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) Dola za Marekani milioni 148.4 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 320 imelielemea shirika hilo.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa imeibua upya mgogoro wa kisheria kati ya Tanesco dhidi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kupitia  uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kuzidiwa huko kwa Tanesco kunatokana na kauli ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kurusha mpira kwa Tanesco, huku akisema shirika hilo ndilo lenye kesi na wanatakiwa kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu sakata hilo.

Kutokanana uamuzi huo MTANZANIA ilimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba ambaye yupo mkoani Kagera katika ziara yake ya kuangalia athari za tetemeko la ardhi ambaye hakupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi wa simu aliotumiwa.

Taarifa kutoka ndani ya Tanesco zinaeleza kwamba timu ya wanasheria wa shirika hilo wamekuwa katika vikao vizito kujadili suala hilo.

“Si hao pia wapo wanasheria nguli pamoja na wale wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wanajadili suala hilo na namna ya kuliendea. Ila naamini baada ya kukamilika kwa kikao chao dira inaweza kupatikana.

“Ila ninachotaka kukuambia suala hili ni zito kwetu na hakuna namna nyingine zaidi ya kujiandaa kwa wanasheria wa Tanesco pamoja na wale wa wizara kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu,” alisema mtoa habari wetu.

Uamuzi wa benki hiyo kulipwa ulitolewa wiki iliyopita na mahakama hiyo, ambapo Tanesco imetakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha  ambacho kinajumuisha riba ya deni la tozo ya uwekezaji.

Suala hilo limeibuka ikiwa imepita miaka mitatu tangu Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini kuruhusu kufanyika kwa malipo ya Dola za Marekani milioni 200 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 300 kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Fedha hizo zilitolewa na kwenda kwa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP) kwenda kwa mmiliki wake, Harbindar Singh Sethi mwenye makazi yake hapa nchini na Afrika Kusini.

Katika kesi hiyo Tanesco ilikuwa inawakilishwa na mawakili wa kampuni za R.K Rweyongeza & Advocates na Crax Law Partners.

Prof. Muhongo bungeni

Novemba  27,  mwaka 2014, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alijibu hoja ndani ya Bunge la 10 na kusema kuwa mjadala wa Escrow, mengi yalisemwa huku akishukuru uchunguzi wa CAG, TAKUKURU.

Alisema miaka ya 90  nchi ilikuwa na upungufu wa umeme kutokana na upungufu wa maji kwenye mabwawa, ambapo 1994 serikali ilitoa kazi ya uwekezaji kwa IPTL ilikuwa iliyokuwa ikimilikiwa na VIP ya Tanzania iliyokuwa na asilimia 30 na Mechmar ya Malaysia yenye asilimia 70.

Alisema Tanesco na IPTL walisainiana mkataba wa miaka 20, hata hivyo uzalishaji haukuanza mara moja kutokana na mgogoro ulioibuka baina yao (Tanesco na IPTL) .

Mwaka 2002  IPTL ilianza kuzalisha umeme na mkataba ukaanza kuhasabiwa hapo, lakini kutokana na mgogoro ikafunguliwa akaunti ya Escrow na mwaka 2004 Tanesco ilifungua shauri kupinga tozo la Capacity Charge

“Taarifa hiyo sio kweli kwani Tanesco haijawahi kufungua kesi yoyote dhidi ya Standard Charted kama ilivyosemwa na PAC. Kesi hiyo ilifunguliwa na Standard charted na ilikuwa haihusu capacity charge.

“Uwiano wa mtaji ni 70 kwa 30 na uamuzi haujabadilishwa na mahakama yoyote. Mwaka 2004 Kampuni ya Mkono &  CO advocates iliishauri Tanesco iendelee kupinga Capacity Charge London. Hata hivyo, Tanesco haikuishauri Tanesco kufungua kesi Tanzania wala mahakama ya Kimataifa.

“Hadi 2013 Jaji Utamwa anatoa hukumu ya mgogoro wa wanahisa wa IPTL kulikuwa hamna kesi yoyote kuhusu tozo ya IPTL,” alisema Profesa Muhongo ndani ya Bunge.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa Serikali ilichukua tahadhari zote  ambapo kwa mujibu wa kinga IPTL itawajibika yakitokea madai yoyote na ilipitiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Inaelezwa kuwa Agosti 2005, benki ya SCB-HK ilinunua kwa bei yapunguzo ya dola za Marekani 76.1 kutoka Benki ya Malaysia ya Danaharta baada ya kushindwa kurejesha deni la muda mrefu kutoka IPTL.

Bei halisi ya deni hilo ilikuwa ni dola milioni 101.7 kwa mujibu wa ushahidi uliopo ambapo IPTL ilikopa dola milioni 100 mwaka 1998 kutoka kwa ubia wa mabenki ya Malaysia ili kujenga mtambo wa kufua umeme wa megawati 100 wa Tegeta.

Chini ya makubaliano hayo SCB-HK ilipewa kandarasi kadhaa ikiwemo haki ya kulipwa deni la 1997, ambapo mkataba wa utekelezaji na hatia ya makubaliano ya dhamana iliyosainiwa na kati ya IPTL na Serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here