SIKU chache baada kuwapo kwa taarifa za kujiondoa kwa benki ya Barclays barani Afrika, benki hiyo imekanusha ikisema itaendelea na kazi kama kawaida, huku ikiwataka wafanyakazi na wateja wake kutokuwa na hofu.
Akitoa taarifa ya fedha ya mwaka 2015 hivi karibuni, Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Jes Staley, alisema benki hiyo inapanga kuuza asilimia 62.3 ya hisa zake barani Afrika kwa kipindi cha miaka miwili hadi mitatu ijayo.
Taarifa hiyo imesema uamuzi huo ulikuwa mgumu kuufanya ikizingatiwa nembo ya benki hiyo katika baadhi ya mataifa ya Afrika ni thabiti.
Staley alitaja sababu ya hatua hiyo ni kushuka kwa faida ya benki kwa asilimia mbili.
Barclays imesema faida yake ya kila mwaka ilishuka asilimia 2 sawa na pauni bilioni 5.4 (Sh trilioni 11.8) kwa mwaka 2015.
Staley alisema pia benki hiyo itapunguza mgawo wake wa faida kwa kila hisa kwa zaidi ya nusu hadi asilimia tatu mwaka 2016 na 2017.
Benki hiyo pia imepunguza fedha inazotenga kama bonasi kwa wafanyakazi wake kwa mwaka 2015 kwa asilimia 10.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Barclays Tanzania, Kihara Maina, alisema kilichotokea ni Barclays PLC kupunguza hisa zake kwa Barclays Africa Group kwa kiasi cha kutoidhibiti kama inavyofanya sasa.
“Kilichofanywa na Barclays PLC inayomiliki asilimia 62.3 ya hisa za Barclays Africa Group Ltd, ni kutoa mikakati yake kwa Bara la Afrika, kwamba kutokana na mikakati ya udhibiti, Barclays kwa miaka miwili mitatu ijayo itapunguza hisa zake kwa Barclays Africa Group kufikia kiwango cha kutoitawala,” alisema Maina.
Alitaja sababu ya kuondoa hisa hizo kuwa ni kutokana na changamoto zinazotokea kwa benki hiyo barani Ulaya na Marekani.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa hatua hiyo haitaathiri benki hiyo kwa Afrika.
“Tunaendelea kusisitiza kuwa tutaendelea kufanya kazi Afrika, tuna matawi nchi 12 za Afrika tukitumikia wateja milioni 12 na wafanyakazi 42,000 Afrika yote. Hiyo yote ni kuonyesha uwekezaji mkubwa tulionao Barclays. Ni miongoni mwa taasisi kubwa za fedha barani Afrika na tutaendelea kuwapo tukiwatumikia wateja,” alisema Maina.
Alisema tangu kuwapo taarifa hizo, hawakuweza kutoa ufafanuzi hadi viongozi wa benki hiyo makao makuu watoe taarifa zao.
“Kitu cha muhimu kujua ni kwamba Barclays Africa Group itaendelea kufanya kazi kama kawaida. BAG Ltd inamiliki asilimia 100 ya benki za Barclays za Tanzania, tunaendelea kufanya kazi kama kawaida, hakuna kinachobadilika,” alisema Maina.
Alisema hakutakuwa na ubadilishwaji wa hisa za BAG katika nchi yoyote ya Afrika ambayo Barclays inafanya kazi.