24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda: Matusi ninayotukanwa yananipa raha

Paul MakondaVERONICA ROMWALD NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, amesema matusi anayotukanwa na baadhi ya watu, hasa kwenye mitandao ya kijamii juu ya wazo lake la kutaka walimu wa wilaya hiyo kusafiri bure katika daladala, alilotoa mwishoni mwa wiki yanampa raha.

Alisema matusi hayo yanamfurahisha na wala hajali kwa sababu yanamsaidia kufikiri zaidi namna ambavyo ataweza kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wake.

Akizungumza katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Redio Clouds FM, Makonda alisema hadi kufikia uamuzi huo amekutana na wadau mbalimbali.

“Tatizo hapa tunachanganya wajibu wa Serikali, wajibu wa mwalimu na wajibu wa wananchi…. Hili jambo halijafanywa na Serikali, naomba nieleweke.

“Maana nimepita kwenye mitandao ya kijamii watu wanatukana, moja ya kitu ambacho kinanipa raha ni matusi ya watu, unajua mtu anapokutukana anakusaidia kufikiri zaidi na anakusaidia wewe uwe mkubwa zaidi kuliko yeye,” alisema.

Alisema anatambua walimu wana madai mengi ikiwamo mshahara mdogo na makato mbalimbali, hivyo uamuzi wake ni kutaka kusaidia kuwapunguzia matatizo.

“Natambua mchango wa walimu na thamani yao kwa jamii, nikasema wakati tunasubiri kukamilika kwa mkakati wa rais ambao utategemea kipato tunachopata kulingana na makusanyo katika suala la mgawanyo wa mshahara, nikaona ni wakati wa kumsaidia nikiwa msaidizi wake kwa nafasi yangu.

“Hatuwezi kusubiri hadi rais aje atoe maelekezo eti hata kwa walimu tufanye hili au tuache hili.

“Nilikutana na baadhi yao wakanieleza wana maisha magumu. Kila ifikapo mwisho wa mwezi mshahara wao ni mdogo na wanajikuta wamekopa na wanakuwa na makato mengi yanayofanya mshahara wao usitoshe ikizingatiwa hapa Dar es Salaam gharama za nyumba ni kubwa.

“Unakuta mwalimu analazimika kwenda kupanga nje ya mji ili aweze kumudu gharama za nyumba, anapokwenda huko anajikuta analazimika kulipia gharama ya nauli iliyogawanyika  makundi mawili,” alisema.

Alisema aliwatafuta wadau wa vyombo vya usafiri na alipowaeleza wazo lake, walikubaliana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles