NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM
BODI ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imetakiwa kuhakikisha inaifumua upya bandari hiyo kwa kutokomeza ufisadi na ajira za kurithishana.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa alikuwa akizungumza Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bodi mpya mamlaka hiyo.
Alisema mifumo ya bandari hiyo na uongozi uliokuwapo ulisababisha bandari kupoteza mabilioni ya fedha na kuisababishia serikali hasara.
Mbarawa alisema michezo michafu ya kupeana ajira za kurithishana nayo imekuwa kichocheo cha wafanyakazi wasio na uwezo ndani ya bandari hiyo ambao hawana uwezo wa kuzalisha kwa manufaa ya kampuni.
Alisema ripoti ya uchunguzi dhidi mwenendo wa bandari hiyo iliyofanywa na wataalam imekamilika na imebaini madudu mengi.
Waziri alisema ataikabidhi ripoti hiyo kwa bodi hiyo iweze kuwawajibisha wahusika wote kwa kuwahamisha vituo vya kazi.
“Ripoti ninayo tayari na nitaikabidhi kwa bodi na kuna vigogo watatu waliosimamishwa wametajwa kwenye ripoti hiyo na wanahangaika kurejea kazini, hivyo naagiza bodi hakikisheni watu hawa hawarejei kwa sababu wanatumia hata fedha kujaribu kurejea.
“Inasikitisha sana kwa kuwa hata mimi nimefuatwa zaidi ya mara mbili na watu hawa ili wanilaghai lakini sitaki kuonana nao kwa kuwa watu hawa ni wala rushwa.
“Hawa ndiyo walioisababishia serikali ipoteze mapato kutokana na mifumo mibovu waliyoitengeneza, kinachowasukuma warejee ni nini hapa jamani?”alisema Mbarawa.