25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Bandari ya Kasanga kunufaisha wafanyabiashara

Na ESTHER MBUSSI -RUKWA

WASAFIRISHAJI wa mizigo na wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo, hususani saruji kwenda nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), watanufaika na biashara hiyo baada kukamilika kwa upanuzi wa gati la kisasa katika Bandari ya Kasanga mkoani hapa.

Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kwa gharama ya Sh bilioni 4.764, unatarajia kukamilika mwakani ambao pamoja na mambo mengine utawezesha bandari hiyo kufanya kazi zake kwa ufanisi na kuongeza mapato kutokana na kuongeza idadi ya meli zinazokuja na kuondoka nchini kupakia na kupakua shehena na abiria. 

Meneja wa Bandari ya Kigoma anayesimamia bandari zote za Ziwa Tanganyika, Ajuaye Msese, alisema jana kuwa kwa sasa bandari hiyo ina gati lenye urefu wa mita 20, lenye uwezo wa kupokea meli moja huku mkakati wa TPA ukiwa ni  kuongeza gati lenye urefu wa mita 100 na kufikia mita 120, litakalowezesha kupokea meli tatu za mizigo na abiria kwa wakati mmoja na hivyo kuondoa msongamano wa meli bandarini hapo.

“Bandari hii ndiyo inategemewa na nchi za Congo na Burundi katika kusafirisha saruji kutoka Mbeya, kwa hiyo upanuzi wa bandari hii kwa ujumla utakaogharimu Sh bilioni 4.7 utawezesha shehena kubwa ya saruji kusafirishwa kwenda nchi hizo kutoka tani 20,000 kwa mwaka hadi tani 100,000 kwa mwaka.

“Bidhaa kubwa inayosafirishwa kwenda nchi za Congo na Burundi ni saruji ambayo inazalishwa na Kiwanda cha Saruji cha Mbeya (Mbeya Cement), hivyo tunatarajia mizigo itakayosafirishwa itaongezeka mara tano zaidi,” alisema.

Aidha, Msese alisema kuboreshwa kwa bandari hiyo, inayotegemewa na mikoa ya Katavi, Mbeya, Songwe na Rukwa utawezesha kukuza uchumi wa taifa. 

Alisema pia upanuzi wa gati hilo utaenda sambamba na ujenzi wa sakafu ngumu, nyumba za wafanyakazi, ghala kubwa la kuhifadhia shehena ya mizigo na ofisi za taasisi za Serikali zinazofanya kazi na bandari.

Msese pia alisema kuwa changamoto ya miundombinu ya barabara ya kutoka Namanyere kuelekea Kisanga imetatuliwa  ambapo tayari imeanza kujengwa na Wakala wa Barabara (Tanroads) ili kufikika kirahisi.

Akizungumzia mapato, alisema kwa sasa ni Sh bilioni moja, na wanatarajia yataongezeka maradufu baada ya kukamilika mradi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles