32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Banana yupo sana tu, hujamtafuta…

981069_579665945398176_1804557359_o2

Na BEATRICE KAIZA,

ALIIBULIWA na Shindano la Pop Idol mwaka 2002, ambapo kwenye fainali za kinyang’anyiro hicho alitamba na wimbo wa My Love wa Westlife. Baada ya hapo, nyota yake ikaanza kung’ara.

Ni miongoni mwa wasanii wachache wa Bongo Fleva,  waliothubutu kuimba wakati ambao Rap ikitamba na kukubalika zaidi – wakati ambao wasanii wa kuimba waliitwa wabana pua, lakini hakukata tamaa, akakaza msuli.

Banana Zahir Ally Zorro, katika kipindi hicho aliweza kupenyeza na kukubalika akiwa na wabishi wengine kama Mr. Paul na baadaye kuunda kundi la B Love M akiwa na memba mwenzake Masiga.

Singo za Anakudanganya na Big Boss ndizo zilizomuweka kwenye ramani ya muziki huo, ambapo albamu yake ya kwanza kumtoa ilikuwa ni Banana, kisha baadaye akaachia Subira, akazidi kuwa kileleni.

Katika kuonyesha kuwa yeye ni kiraka, kwa nyakati tofauti amewahi kufanya kazi na Bendi ya Inafrika, Bushoke na Soul Faith.

Unakumbuka vibao vikali kama Nimekuchangua Wewe, Mama Yangu, Haohao, Niko Radhi, Nataka Niwe Nawe, Safari, Mapenzi ya Simu, Mama Kumbena, Zoba na nyinginezo?

Kwanini Banana siku za hivi karibuni amekuwa kimya sana? Yuko wapi? Hayo ni kati ya mambo yaliyomfanya polisi wa Swaggaz amsake usiku na mchana hadi alipofanikiwa, ambapo Banana alitoa kauli moja tu: “Nipo sana tu, hukunitafuta.”

Swaggaz: Uko wapi sasa Banana, kimya sana. Watu wanakutafuta, wakuone wapi?

Banana: Kama unavyojua zangu ni muziki wa bendi, naendelea vizuri tu. Napiga na B Band pale Q Bar, Masaki kila Alhamisi na Slipway Hotel kila Ijumaa, nikiwa na timu yangu Maneno Uvuruge, Ismail Kipara, Chriss Music, Mc Mt na wengine. Watu waje wale muziki wa kistaarabu.

Swaggaz: Inamaana hutatoa albamu tena au singo yoyote mpya redioni?

Banana: Hapana… bado nipo kwenye game na kuna kazi nyingi zinakuja, mashabiki wangu wakae mkao wa kula,  mwishoni mwa Novemba natoa wimbo mpya uitwao ‘Niamini’. Ni moto wa kuotea mbali.

Swaggaz: Unadhani kwanini wasanii wa Tanzania wanakwepa kupiga muziki wa live?

Banana: Tatizo wasanii wa Tanzania, baadhi wanaogopa kujaribu muziki wa live ingawa wapo wanaofanya vizuri kama Ali Kiba, Barnaba na Ruby.

Swaggaz: Kwa maoni yako ni wasanii gani ambao kwa sasa wanafanya vizuri zaidi kwenye Bongo Fleva?

Banana: Wengi wanajitahidi lakini zaidi naona Diamond, Ali Kiba na Q Chief wanafanya vizuri zaidi.

Swaggaz: Muziki wa Singeli unazidi kukua, wakati huo tunaona wasanii wengine wakubwa wakigeukia muziki huo, mfano Profesa Jay na wengineo, vipi kwa upande wako?

Banana: Mimi nina uwezo wa kufanya kila muziki, lakini Singeli kwangu kwa sasa sijafikiria lakini naona ni muziki mzuri ambao unakuja vizuri, wasanii wake wakiutumia vema unaweza kutoka kimataifa na kuipaisha zaidi  Tanzania.

Swaggaz: Unadhani mabifu kwa wasanii, yawe ya kweli au ya kutengeneza, yanakuza muziki?

Banana: Wasanii wa sasa siyo wabunifu, wavivu kujituma na akili zao wameziweka kwenye mabifu tu ambayo hayawezi kukuza muziki zaidi ya kuudidimiza.

Swaggaz: Nini ushauri wako kwa wasanii wanaotumia madawa vya kulevya?

Banana: Utumiaji wa madawa za kulevya siyo fasheni, ila tatizo Watanzania wanapenda kuiga vitu ambavyo havina maana.

Wasanii ambao bado wanatumia madawa ya kulevya wanatakiwa kubadilika na kufanya mambo ya kuendeleza maisha yao na kukuza vipaji vyao vya muziki. Mwisho wa madawa ya kulevya, siku zote siyo mzuri.

Swaggaz: Ushauri mzuri sana Banana, lakini inadaiwa hata mdogo wako, mwanamuziki Maunda Zorro, naye ametumbukia kwenye wimbi la madawa ya kulevya. Unaliongeleaje hilo?

Banana: Hayo madai ya Maunda kutumia madawa ya kulevya ni maneno tu ya watu. Inakuwaje mtu atumie na kuacha bila kwenda kwenye matibabu? Siyo kweli, puuza hayo madai.

Swaggaz: Mwisho kabisa Banana, unadhani wasanii kurekodi video nje ya nchi kuna faida?

Banana: Kwangu naona ni sahihi na kuna faida. Ni kati ya njia inayosaidia kukimbizana na soko la kimataifa. Ujue kuna wakati ilifika video za Kibongo karibu zote zikawa kama zinafanana. Sasa hivi angalau ladha zinakuwa tofauti na ushindani mkubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles