Chris Brown azidi kumtesa Karrueche Tran

0
841

chris-brown-and-karrueche-tran-2

Na BADI MCHOMOLO,

MWAKA 2015, msanii wa muziki wa RnB, nchini Marekani Chris Brown alitangaza kupitia mitandao ya kijamii kuwa yeye ni baba wa mtoto mmoja aliyempata na Nia Guzman.

Inasemekana msanii huyo alikuwa hajui kama Nia Guzman alikuwa amempa mimba, lakini alipewa taarifa mara baada ya mtoto huyo kuzaliwa na kufikisha umri wa miezi tisa.

Haikuwa kazi ngumu kwa msanii huyo kukubali kwa kuwa ni mtoto wake wa kwanza, pia ni kweli kwamba alikuwa na uhusiano na mrembo huyo.

Uhusiano wake na Nia Guzman ulikuja mara baada ya Chris kuachana na mpenzi wake, Rihanna mwaka 2013 kutokana na mgogoro wao.

Lakini inadaiwa kwamba Chris na Nia Guzman uhusiano wao haukuwa wa kudumu, Chris alidai kuwa alikutana na mpenzi huyo kwa bahati mbaya.

Warembo wengi walikuwa wanatafuta nafasi ya kuwa mpenzi wa Chris, lakini nafasi hiyo ilikuwa ngumu, baada ya muda aliachana na Nia Guzman na kumpata mwanamitindo Karrueche Tran.

Huu ni uhusiano ambao ulikubalika na wengi ambao wanampenda Chris Brown, kwa kuwa wawili hao walikuwa wanapendeza wakiwa pamoja kama ilivyo awali Chris na Rihanna.

Uhusiano wao ulikuwa wazi, huku watu wakiamini kuwa unaweza kudumu kwa muda mrefu ikidaiwa kwamba Chris amepata sehemu ya kutuliza mawazo yake baada ya kuachana na Rihanna.

Lakini uhusiano huo ulikuja kuvunjika mara baada ya msanii huyo kuletewa mtoto wa miezi tisa na kuambiwa ni wa kwake ambaye anajulikana kwa jina la Royalty.

Hapo ndipo Karrueche alijisikia maumivu makali kwa kugundua kwamba mwenzake tayari ana mtoto lakini hakuambiwa ukweli tangu mwanzo walipoanza uhusiano huo.

Chris alikuwa na furaha ya kupata mtoto, lakini Karrueche hakuwa na amani kwa kuwa alipanga kuwa msichana wa kwanza kuzaa na Chris, lakini ndoto hizo zikawa zimefikia mwisho, akaona bora aachane na msanii huyo.

Hata hivyo wakati Karrueche anaamua kufanya uamuzi huo mgumu wa kuachana na Chris, mrembo huyo alisema kuwa bado ataendelea kumpenda Chris na atakuwa tayari kurudiana kama atabadilika.

Kabla ya kuachana kwa wawili hao, Karrueche aliwahi kusema kwamba msanii huyo hajatulia, amekuwa mtu wa wasichana sana lakini yupo tayari kuvumilia kwa kuwa anampenda.

Hata hivyo baada ya Chris kuachana na Karrueche, msanii huyo hakuweza kumtambulisha mpenzi mpya hadi sasa, wakati huo Karrueche akionekana na wanaume mbalimbali kama vile Memphis Depay ambaye ni mchezaji wa klabu ya Manchester United pamoja na Klay Thompson ambaye ni nyota wa kikapu wa timu ya Golden State Warriors.

Wakati huo Rihanna naye alionekana akiwa na baadhi ya wasanii wa muziki na wachezaji wa kikapu, lakini hatua za mwisho mrembo huyo alidaiwa kutoka na msanii wa Pop nchini Marekani, Drake.

Taarifa ambazo ziko wazi kwa sasa ni kwamba Drake na Rihanna wamemwagana kwa madai kwamba Drake anatoka na mrembo kutoka nchini India ambaye anajulikana kwa jina la India Love.

Baada ya taarifa hizo, habari nyingine zikaeleza kuwa Chris  ameona bora arudiane na mpenzi wake wa zamani Rihanna  baada ya kusikia ameachana na Drake.

Inasemekana kuwa Chris ameanza kutuma zawadi kwa familia ya Rihanna kwa ajili ya kurudisha upendo wa awali.

Kitendo hicho kimemuumiza sana Karrueche ambaye alikuwa anasubiri kauli kutoka kwa Chris ya kutaka kurudiana, lakini baada ya taarifa hizo ameshindwa kuzuia hisia zake na kuweka wazi kupitia akaunti yake ya Instagram.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here