*Yatumia “Kenya Diaspora Forums 2024″ kukutanisha Wakenya waishio nchini
Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Kenya imetajwa kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania ambapo imewekeza zaidi ya Dola Bilioni 2 za Marekani sawa na Sh Trilioni 5 za Tanzania hatua ambayo pia imechochea ajira kwa wazawa.
Hayo yamebainishwa Machi 9, 2024 jijini Dar es Salaam na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Balozi Isaac Njenga katika hafla iliyowakutanisha zaidi ya Wakenya 500 wanaoishi nchini Tanzania “Kenya Diaspora Forums 2024”
Amesema Wakenya wamewekeza zaidi nchini Tanzania huku nchi hiyo ikiongoza kwa idadi ya wageni wanaoingia nchini kutoka kote duniani.
“Kenya ina mchango mkubwa sana katika uchumi wa Tanzania kwani ukiangalia takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba wageni wengi wanaoingia Tanzania kutoka kote duniani Kenya ni kinara hatua ambayo inachochea uchumi kutokana na huduma mbalimbali wanazopata wakiwa hapa nchini ikiwamo usafiri, hoteli, maduka na vingine.
“Ukiacha hiyo kuna wataalamu mbalimbali wanaokuja Tanzania, kwani uwekezaji wa Kenya nchini Tanzania ni zaidi ya dola bilioni 2 huku unaohusisha zaidi ya kampuni 500 yaliyozalisha ajira takribani 100,000 kwa Watanzania, hivyo huu ni uwekezaji mkubwa ulipo hapa unaozidi kutuimarisha sisi kama ndugu na watu wa Afrika Mashariki, badala ya uwekezaji huu kwenda katika nchi nyingine unaongeza mzunguko wa fedha nchini na kuchangia kukuza pato la Taifa la Tanzania,” amesema Balozi Njenga.
Awali, akizungumzia siku hiyo, Balozi Njenga alisema kuwa utaratibu huo unawasaidia kujuliana hali ikiwamo kuwaeleza huduma zinazotolewa na ubalozi huo hapa nchini ikiwamo kujenge undugu na uzalendo ikiwamo utamaduni.
“Kama unavyofahamu Wakenya wanaoshi hapa Tanzania wengine wako na ndugu na jamaa zao huku kukiwa na watoto waliozaliwa hapa, hivyo hii ni fursa ya kuweza kutambuana na kufahamiana pamoja na kukumbushana utamaduni wa Mkenya.
“Sambamba na hilo tunawasaidia kuweza kuhuisha hatia zao za kusafiria kama zimeisha muda wake na kutambulika,” amesema Balozi Njenga.
Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Serikali ya Kenya, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uhusiano na Ushirikiano katika Idara ya Mambo ya Nje ya Diaspora, Ann Wanjohi, aliwataka Wakenya wanaoishi Ughaibuni kuwekeza zaidi nyumbani na kutafuta nafasi zaidi za kazi kwa Wakenya walio ng’ambo.
“Nawaomba muunde vyombo vya uwekezaji vitakavyowasaidia kujikwamua kiuchumi. Kwa kujenga mitandao hii, unajenga hali ya kuhusishwa na mshikamano,” alisema.
Aliwataka zaidi kujihusisha na ustadi na uhamishaji wa teknolojia na kufungua njia za biashara kwa bidhaa na huduma za Kenya katika nchi wanazopokea.
Huku ikitambua kujitokeza kwa wingi kwa Wakenya wanaoishi Tanzania katika hafla hiyo, idara ya Diaspora ilisisitiza kuwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa mataifa na wasio wa serikali utatoa miundo na mifumo ya kusaidia diaspora katika kutumia uwezo wao mkubwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Kenya.