KULWA MZEE – DAR ES SALAAM
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi inaombwa kutengua uamuzi uliotolewa na Baraza la Nyumba la Kilombero, uliowapa umiliki wa shamba la hekari 40 Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Maombi hayo yapo katika rufaa iliyokatwa na Alphonce Kakweche na Mgainamba Kihakwi wakipinga uamuzi dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Bakwata.
Rufaa hiyo iliyopangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Dk. Modesta Opio, warufani wanapinga uamuzi uliotolewa na baraza hilo la ardhi Februari 8 mwaka 2017, wakidai kuwa ardhi hiyo ni urithi wa Kakweche kutoka kwa wazazi wake tangu miaka ya 1990.
Warufani wanadai sababu za kukata rufaa ni kwamba Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kilombero lilikosea kusikiliza shauri hilo kwa kuwa halikuwa na mamlaka.
“lilikosea kisheria na kimkakati kutoa hukumu ikiwapendelea Bakwata bila kuzingatia maoni ya wazee wa baraza kama inavyotakiwa kisheria na bila kuzingatia ushahidi.
“Baraza hilo lilikosea kuona kuwa ardhi inayobishaniwa ilikuwa imetelekezwa na wajibu rufani na kwamba walifuata taratibu zote za kisheria zinazotakiwa kabla ya kupata shamba hilo,” walidai.
Wajibu rufani katika majibu yao wanapinga hoja hizo huku wakidai Baraza la Ardhi na Nyumba lilikuwa na mamlaka kisheria ya kusikiliza shauri hilo.
Wanadai ushahidi wa Bakwata ulibainisha kuwa wao ndio wamiliki halali wa eneo hilo na hivyo ilikuwa hahali na sahihi kuamua kuwa ardhi hiyo ilitelekezwa na wajibu rufani.
Kwamba uamuzi uliotolewa na Baraza la Ardhi ulikuwa sahihi na hivyo wanaomba rufaa iliyokatwa na warufani itupiliwe mbali.