24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Bajeti yaweka kando bia, sigara

bajetiNA WAANDISHI WETU, DODOMA/DAR
WAZIRI wa Fedha, Saada Mkuya Salum, amewasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/16 ya Sh trilioni 22.1 huku kwa mara ya kwanza ikiwa haijapandisha kodi ya sigara na vileo kama ilivyokuwa kwa miaka iliyopita.
Akiwasilisha mapendekezo hayo jana bungeni mjini Dodoma, Waziri Saada alisema kwa mwaka huu wa fedha bajeti hiyo itajikitaka katika kutekeleza vipaumbele vya Uchaguzi Mkuu, msukumo katika kukamilisha miradi inayoendelea sasa, msukumo maalumu kwenye miradi ya umeme na maji vijijini pamoja na kuimarisha rasilimali watu.

FEDHA ZA MIRADI
Waziri Saada alisema sekta ya nishati na madini imetengewa Sh bilioni 916.7 sawa na asilimia 5.7 ya bajeti yote bila kujumuisha Mfuko Mkuu wa Serikali.
Alisema kati ya fedha hizo, sh bilioni 447.1 zimetengwa kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa umeme vijijini.
“Miundombinu – sekta ya ujenzi na uchukuzi shilingi bilioni 2,428.8 sawa na asilimia 15.1 ya bajeti yote bila kujumuisha Mfuko Mkuu wa Serikali. Kilimo shilingi bilioni 1,001.4 sawa na asilimia 6.2, elimu shilingi bilioni 3,870.2 sawa na asilimia 24.0 .
“Pia maji imetengewa shilingi bilioni 573.5 sawa na asilimia 3.6 ya bajeti yote, pamoja na sekta ya afya ambayo imetengezwa shilingi bilioni 1,821.1 sawa na asilimia 11.3 ya bajeti yote, ambapo zimetengwa fedha hizo kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa madawa, kuzuia magonjwa ya mlipuko, chanjo za watoto, ujenzi wa zahanati na kudhibiti Ukimwi na malaria,” alisema Waziri Saada.

VIPAUMBE VYA BAJETI
Waziri Saada alitaja vipaumbe vya bajeti ya mwaka 2015/16 ambavyo ni kugharamia shughuli za Uchaguzi Mkuu ikiwa ni pamoja na gharama zote za shughuli za Bunge lijalo, mabaraza ya madiwani, shughuli za Serikali awamu ya nne na kuanza kazi kwa Bunge lijalo.
Alisema kipaumbele cha pili ni kuweka msukumo katika kukamilisha miradi inayoendelea na tatu, kuweka msukumo maalumu kwenye miradi ya umeme na maji vijijini na kuimarisha rasilimali watu. Ili kutekeleza hayo, msisitizo mkubwa utawekwa kwenye kukusanya mapato ya ndani.

MAREKEBISHO YA MFUMO WA BAJETI
Waziri Saada alisema Serikali imefanya marekebisho ya mfumo wa bajeti ambapo kwa mwaka wa fedha 2015/16 imepanga bajeti ya mapato na matumizi yenye jumla ya Sh bilioni 22.1.
Bajeti hiyo imeongezeka kwa Sh bilioni 2.2 ikilinganishwa na bajeti ya Sh bilioni 19.3 ya mwaka wa fedha 2014/15.
Waziri Saada alisema baada ya majadiliano ya kina na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, walikubaliana na tahadhari ya kamati kwamba maoteo ya mapato ya kodi yaliyotumika katika mfumo huo hayaendani na mwenendo wa makusanyo ya miaka ya karibuni.
“Kamati ya Bajeti ilipendekeza Serikali ipunguze ukubwa wa bajeti na kushusha maoteo ya mapato yatokanayo na kodi, ilishauri kwamba pamoja na matumaini ya Serikali ya kuweza kufikia lengo la makusanyo lililowekwa, iliona itakuwa busara kupunguza matumizi hadi hapo lengo la mapato la awali litakapofikiwa, ambapo Serikali itabidi kurudi bungeni kuomba kibali cha matumizi ya ziada.
“Kama nilivyoeleza, tulikubaliana na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti kwa sababu bado kuna fursa ya kurudi bungeni katikati ya mwaka wa fedha endapo makusanyo yaliyokusudiwa yatafikiwa na kuomba kibali cha kurudisha fedha ambazo zimepunguzwa kwenye mafungu katika mfumo wa bajeti unaopendekezwa sasa,” alisema Waziri Saada.
Alisema pamoja na kupunguza fedha kwenye mafungu, wameongeza nakisi ya bajeti kufikia asilimia 4.2 ya Pato la Taifa ili kuiwezesha Serikali kulipa malimbikizo yote yaliyohakikiwa ya madai ya makandarasi, wazabuni, watumishi wa Serikali pamoja na sehemu ya deni la Mfuko wa Pensheni wa PSPF kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Saada alisema kutokana na maelezo hayo, mfumo wa Mapato na Matumizi aliouwasilisha una mapato ya Sh bilioni 22.5 ambapo mapato ya kodi ni shilingi bilioni 12,363 na mapato yasiyo ya kodi shilingi bilioni 1,112.7.

KUONGEZA MAKUSANYO YA MAPATO
Akiwasilisha mapendekezo hayo, Waziri Saada alisema pamoja na Serikali kurekebisha mfumo wa bajeti kwa tahadhari, bado ina dhamira ya kuhakikisha kwamba katika mwaka ujao wa fedha, makusanyo ya kodi yanaongezeka.
Alisema kwa sasa makusanyo ya mapato ya kodi ni takribani asilimia 12 ya Pato la Taifa, kiwango ambacho ni cha chini ikilinganishwa na nchi nyingi jirani.
“Nina uhakika kuwa tunao uwezo wa kuongeza mapato ya kodi, tutafanya hivyo kwa kuwa na mikataba ya utendaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yaani ‘performance contracts’, kuanzia ngazi ya juu mpaka wasimamizi wa chini ili kuhakikisha tunafikia malengo ya ukusanyaji,” alisema.
Alisema utendaji wa TRA na hasa wa watendaji wenye mamlaka ya usimamizi utapimwa kwa namna wanavyofikia malengo yao ya ukusanyaji wa mapato ya kodi.
Aliongeza kuwa Serikali pia itaongeza jitihada za kuziba mianya ya kukwepa kodi na kuongeza matumizi ya mifumo ya Tanzania Customs Integrated System yaani TANCIS, pamoja na mfumo mmoja wa ukadiriaji wa thamani za bidhaa, yaani Centralized Price-Based Valuation System kwa Jamhuri ya Muungano ambayo yatapunguza ukwepaji wa kodi.
Alisema mifumo hiyo pia itaondoa ulazima wa TRA kukadiria thamani ya bidhaa zinazoingia Tanzania Bara kutokea Zanzibar ikiwa hiyo ni hatua kubwa sana katika kumaliza kero ya Muungano kwa waingizaji wa bidhaa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.
Waziri Saada alisema hatua nyingine zitakazochukuliwa ili kuongeza mapato ni kupiga marufuku Serikali kutumia wazabuni ambao hawalipi kodi kikamilifu.
“Serikali, Wakala wa Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa hazitafanya biashara na mzabuni yeyote ambaye hatumii mashine za EFD,” alisema.
Aliongeza jitihada za kuongeza mapato zitasaidia pia kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali kwa fedha za wahisani na kusisitiza kiwango cha utegemezi kimepungua kutoka asilimia 24 mwaka 2004/05, asilimia 17 mwaka 2010/11, na kufikia asilimia 6.4 mwaka 2015/16.

MISAMAHA ILIYOFUTWA
Kutokana na bajeti hiyo, Serikali imetangaza kufuta misamaha ya kodi kwa bidhaa zenye umuhimu wa kipekee zikiwamo pembejeo, zana za uvuvi, vifaa tiba pamoja na bidhaa zote za mitaji na kusema mwananchi atakaponunua bidhaa hizo hatatozwa kodi.
Saada alisema misamaha hiyo inalenga kuinua mapato ya wananchi wa kawaida ambao hutegemea shughuli za kilimo na uvuvi.
“Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ambayo itaanza kutumika Julai Mosi mwaka huu, Serikali itaondoa kodi kwa bidhaa muhimu kama vile pembejeo, zana za uvuvi, vifaa tiba na bidhaa zote za mitaji,” alisema Saada na kuongeza:
“Huu ndio mwelekeo wa mageuzi tunayoyafanya katika kupunguza misamaha ya kodi inayotolewa kwa ridhaa (discretionary). Kaulimbiu ya mageuzi haya ni ‘Punguza ridhaa ongeza bidhaa’, yaani kupunguza misamaha ya kodi inayotolewa kwa ridhaa na badala yake kupunguza kodi kwenye bidhaa zenye umuhimu maalumu kwa wananchi na uchumi itakayotolewa moja kwa moja kwenye sheria.”
Alisema lengo kuu ni kuhakikisha usawa, haki na ufanisi katika kodi na kupunguza mianya ya upendeleo na hata rushwa katika utoaji wa misamaha ya kodi kwa ridhaa.
Aliongeza kuwa pamoja na mwelekeo huo wa kupunguza misamaha ya kodi kwa ridhaa, bado Serikali inatambua umuhimu wa kutoa misamaha ya kodi kimkakati kwa kipindi maalumu ili kuvutia wawekezaji wakubwa wanaowekeza fedha nyingi na kuzalisha ajira kwa Watanzania.
Aidha alisema misamaha hiyo itatolewa kwa uwazi na kutakuwapo na ufuatiliaji, tathmini na uwajibikaji wa kutosha ambapo Serikali imeweka mapendekezo kwenye Muswada wa Fedha wa mwaka 2015/16 wa namna ya kutambua wawekezaji mahsusi wa kimkakati ambao wataweza kupewa misamaha mahsusi ya kodi itakayopendekezwa na Waziri wa Fedha na kupata idhini ya Bunge.
Alitaja sifa za mwekezaji mahsusi wa kimkakati ikiwa ni pamoja na kuwa na mtaji usiopungua dola za Marekani milioni 300 na mtaji wa kifedha upitie kwenye taasisi za fedha nchini ikiwa ni pamoja na huduma za bima.
Huku uwekezaji huo ukitakiwa kuleta ajira kwa Watanzania zisizopungua 1,500 pamoja na Wawekezaji hao kuhakikisha wanazingatia Sera ya Uwezeshaji ya mwaka 2004 na kutumia huduma na bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Tofauti na awali Waziri Saada alisema Wizara ya Fedha itatangaza misamaha yote ya kodi inayoitoa kupitia tovuti yake ili kila mwananchi ajue sababu na ni nani ananufaika na misamaha hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles