27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri wa JK ahesabiwa kwa Lowassa

maseleNA ELIAS MSUYA, DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Steven Masele, ametangaza kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika harakati zake za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Masele aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kabla ya Baraza la Mawaziri kuvunjwa, jana aliibukia katika mkutano wa kutafuta wadhamini wa Lowassa uliofanyika mjini Shinyanga na kusema sasa kada huyo wa CCM anasubiri kupitishwa na vikao vya chama.
Akizungumza katika mkutano huo, Masele ambaye pia ni mbunge wa Shinyanga Mjini, alisema yeye pamoja na wana CCM wenzake wanasubiri Kamati Kuu ya CCM ifanye kazi yake kisha wamalizie kumpitisha Lowassa.
“Tanzania yote inajua,” alisema Masele na kuuliza “inajua haijui…?” huku akijibiwa na wana CCM, “Inajuaaa…”
“Tanzania inajua na dunia nzima inajua kwamba Lowassa yuko hapa. Mimi ni mjumbe wa Mkutano Mkuu, wa NEC wetu wamesema hapa, sisi tumekaa mkao wa kula tunasubiri wafanye kazi yao na sisi tunamalizia kupiga bao tu,” alisema Masele.
Mbali na Masele, mawaziri wengine walioonyesha kumuunga mkono Lowassa kwa nyakati tofauti ni pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto, Sophia Simba na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Nyerere aliyemsindikiza kuchukua fomu mjini Dodoma.
Katika mkutano huo, alikuwapo pia Mbunge wa Msalala ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ambaye alimsifia Lowassa kwa utendaji bora alipokuwa Waziri Mkuu na hasa kuwaletea maji wakazi wa Mkoa wa Shinyanga.
“Sisi wananchi wa Mkoa wa Shinyanga tuna imani na wewe kwa jambo moja ulilotufanyia. Ulileta maji kutoka Ziwa Victoria. Shinyanga ilikuwa jangwa, lakini ulileta maji, sisi watu wazima tuliona kwa macho,” alisema Maige.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, alisema Lowassa ni miongoni mwa viongozi walioandaliwa tangu enzi za Mwalimu Nyerere.
“Kuna wakati chama kiliwaandaa vijana wake kwa kuwapeleka chuo kikuu ili wawe viongozi wa baadaye, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, Lowassa na wengineo nawahifadhi. Sasa umefika wakati wa Lowassa…,” alisema Guninita.
Katika mkutano huo, Lowassa alivunja rekodi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kupata wanachama 7,014 waliojitokeza kumdhamini.
Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga, Charles Sangula, alisema kati ya wanachama hao, 3,221 walitoka katika wilaya yake, 2,610 Kishapu na 1,183 Kahama.
Naye Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Kanali Maulid aliwataka makada wa chama hicho kutochafuana kwa kashfa wakati huu wa uchaguzi, na kuchagua mtu anayekubalika ndani na nje ya chama.
“Tumchague mtu anayekubalika ndani na nje ya chama chetu. Lowassa anakubalika. Lakini wako baadhi ya makada wanaochukua fomu na kuanza kuwachafua wenzao. Nashukuru Lowassa hakufanya hivyo,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema kulingana na matokeo ya utafiti uliofanywa na asasi yake ya Tanzana Mzalendo Foundation, Lowassa amekidhi vigezo vyote 10 vya uongozi bora.
“Tuna taasisi yetu ya Tanzania Mzalendo Foundation, tumeweka vigezo 10 na vyote Lowassa amepata asilimia 100. Baadhi ya vigezo hivyo ni uzalendo, uvumilivu na kuwa na uamuzi mgumu,” alisema Mgeja.
Akizungumza na wana CCM waliokusanyika katika ukumbi huo, Lowassa aliwashukuru na kurudia sababu yake ya kugombea urais.
“Nimerudi nyumbani kuwaambia kuwa nimeanza safari ya matumaini. Nilikuwa hapa mwaka 1977 hadi 78, mlinilea vizuri.
“Nimegombea kwa sababu nimechoshwa na umasikini. Mwaka 1962, Mwalimu Nyerere alitaja maadui watatu wa Tanzania kuwa ni ujinga, umasikini na maradhi. Lakini hadi leo kuna viongozi wa Tanzania wanajivunia umasikini. Kazi ya kiongozi ni kuwatoa watu kwenye umasikini na kuwapeleka kwenye utajiri,” alisema Lowassa.
Aliwataka pia wana CCM kujiandikisha ili wawe na sifa ya kupiga kura.
Lowassa aliingia Shinyanga saa sita mchana kwa ndege akiwa na msafara wake kisha wakaelekea kwenye ofisi ya CCM mkoa na baadaye ofisi ya wilaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles