Elizabeth Hombo-Dar es Salaam
SERIKALI imesema bajeti ya 1920/20 inalenga kuimarisha sekta ya uzalishaji na kilimo kwa lengo la kujenga uchumi wa viwanda.
Pia imefanya marekebisho mbalimbali ya tozo na kodi kwa lengo la kuondoa kero kwa wafanyabiashara na wazalishaji.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akiwasilisha bajeti hiyo bungeni Dodoma jana, alisema kipaumbele chake cha pili ni ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.
Vilevile, alisema Serikali inatarajia kufanya mabadiliko mbalimbali ya sheria za kodi ili kuwa na mfumo tulivu wa kodi.
Katika marekebisho hayo, Serikali imesamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kwenye makasha yenye majokofu yanayotumika kwenye kilimo cha kisasa cha mboga mboga.
Dk. Mpango alisema Serikali pia imesamehe VAT kwenye vifaa vya kukaushia nafaka.
“Msamaha huu unatarajiwa kutoa unafuu kwenye gharama za kukausha nafaka kwa ajili ya kuzihifadhi. Aidha, hatua hii itachochea ukuaji wa kilimo cha mazao ya nafaka,” alisema.
UMEME Z’BAR
Aidha, Dk. Mpango alisema Serikali imepunguza VAT kutoka asilimia 18 hadi sifuri kwenye huduma ya umeme unaouzwa kutoka Tanzania Bara kwenda visiwani Zanzibar.
VILAINISHI VYA NDEGE
Dk. Mpango alisema Serikali imetoa msamaha wa VAT kwa vilainishi vya ndege vinavyoingizwa nchini na waendeshaji wa ndani.
TAULO ZA KIKE
Alisema Serikali imefuta msamaha wa VAT uliokuwa unatolewa kwenye taulo za kike kwa kuwa haujawezesha kupatikana kwa bidhaa hiyo muhimu kwa bei nafuu kwa walengwa na badala yake unawanufaisha wafanyabiashara.
“Wakati Serikali ilipoweka msamaha huu, ilitarajia kuwa wazalishaji wa taulo za kike wataziuza kwa bei nafuu baada ya kusamehewa kodi,” alisema Dk. Mpango.
Aidha, Dk. Mpango alisema Serikali imefanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332, ambapo imepunguza Kodi ya Mapato ya Makampuni kutoka asilimia 30 hadi 25 kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2019/20 hadi 2020/21 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya kuzalisha taulo za kike.
“Serikali itaingia mkataba wa makubaliano na kila mwekezaji ambao utaainisha wajibu wa kila upande. Lengo la hatua hii ni kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu, kuongeza ajira na mapato ya Serikali.
“Hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje na kuhamasisha uzalishaji wake ndani ya nchi,”alisema Dk. Mpango.
KODI YA ZUIO
Dk. Mpango alisema Serikali imasamehe Kodi ya Zuio inayotozwa kwenye gharama zinazoambatana na mikopo kama ada za bima, gharama ya usimamizi na uandaaji wa mkopo.
Alisema gharama hizo ni pamoja na ada nyingine zinazoendana na gharama za mkopo.
“Kutoa msamaha wa kutengeneza hesabu ambazo zinatakiwa kuwasilishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya ukokotoaji wa kodi ya mapato kutoka kiwango cha sasa cha Sh milioni 20 hadi Sh milioni 100.
“Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama kwa mlipakodi ya kutafuta mtaalamu kwa ajili ya kutengeneza hesabu. Aidha, hatua hii inalenga pia kuchochea ulipaji kodi wa hiari na kuongeza mapato ya Serikali,” alisema.
Dk. Mpango alisema Serikali imesamehe kodi kwenye mauzo ghafi yasiyozidi Sh milioni 4 kwa wenye vitambulisho vya wajasiriamali na kupunguza kiwango cha chini cha kodi kutoka Sh 150,000 kwa mwaka hadi Sh 100,000 kwa mwaka.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kupunguza mzigo wa kodi kwa walipakodi wadogo pamoja na kuoanisha viwango vya kodi na kiwango cha chini kinachotakiwa kwa mfanyabiashara kutumia Mashine ya Kodi ya Kielektroniki (EFD) ambacho kwa sasa ni Sh milioni 14.
Dk. Mpango alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Kifungu cha 124(2), marekebisho ya viwango maalum vya ushuru wa bidhaa kwa bidhaa zote zisizo za petrol, yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla.
Alisema kwa msingi huo wa sheria, alipendekeza kutokufanya mabadiliko ya viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa kwa bidhaa zote zisizo za petroli.
Dk. Mpango alisema hatua hiyo inazingatia kiwango kidogo cha mfumuko wa bei nchini na lengo la Serikali kujenga uchumi wa viwanda, hivyo kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.
Alisema Serikali inapendekeza kurekebisha sheria ya ushuru wa bidhaa kwa bidhaa chache tu kama kupunguza ushuru wa bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kutokana na usindikaji wa matunda.
“Matunda hayo ni kama ndizi, mabibo, rozela/choya, nyanya yanayozalishwa hapa nchini tofauti na zabibu kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 kutoka Sh 200 kwa lita hadi Sh 61 kwa lita ikiwa ni punguzo la Sh 39 kwa lita.
“Lengo la hatua hii ni kuhamasisha ulipaji wa kodi wa hiari na pia kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vidogo vidogo vya aina hii. Aidha, bei ya mvinyo huu kwa lita inafanana na bei ya vinywaji baridi,” alisema.
NYWELE BANDIA
Vilevile, Dk. Mpango alisema Serikali itatoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye nywele bandia zinazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
MABOMBA, VIFAA VYA PLASTIKI
Serikali inapendekeza kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye bidhaa za mabomba na vifaa vya plastiki vinavyotumika kwenye ujenzi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya maji kwa kuwa hivi sasa kuna viwanda vingi vyenye uwezo wa kuzalisha bidhaa hizo na kutosheleza mahitaji hapa nchini.
“Hatua hii inahusisha bidhaa za mabomba na plastiki zinazotambuliwa katika HS Code 39.17. Lengo la kuanzisha ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa hizo ni kulinda viwanda na kuongeza fursa za kazi, ajira na mapato ya Serikali,” alisema.
Alisema ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh bilioni 2.9.
Akizungumzia kuhusu Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura 438, alisema Serikali inapendekeza kuongeza muda wa miezi sita kwa walipakodi waliokubaliwa kulipa kodi wanazodaiwa.
Alisema hatua hiyo ya marebisho ya sheria inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh bilioni 367.
LESENI YA UDEREVA
Dk. Mpango alisema Serikali inapendekeza kuongeza tozo ya leseni ya udereva kutoka Sh 40,000 hadi Sh 70,000 huku ikiongeza ada ya kadi ya usajili wa magari kutoka Sh 10,000 hadi Sh 50,000.
Kwa upande wa pikipiki za matairi matatu kutoka Sh 10,000 hadi Sh 30,000 na pikipiki kutoka Sh 10,000 hadi Sh 20,000.
Alisema hatua hizo kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh bilioni 18.1.
USHURU WA FORODHA
Alisema Serikali inapendekeza kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwenye malighafi ya kutengeneza taulo za watoto zinazotengenezwa hapa nchini kwa mwaka mmoja.
“Kupunguza ushuru wa forodha kutoka kiwango cha asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifaa vinavyotumika katika kukata, kung’arisha na kuongeza thamani ya madini ya vito.
“Kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye makaratasi yanayotumika kama malighafi ya kutengeneza vifungashio vya mboga mboga kwa ajili ya kuuza nje ya nchi,” alisema.
Dk. Mpango alisema kwa kuwa mbogamboga zinalimwa kwa wingi hapa nchini, alipendekeza kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi 35 kwa mwaka kwa mboga zinazotoka nje.
“Kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye soseji na bidhaa za aina hiyo,” alisema.
Alisema kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 35 badala ya 25 kwa mwaka mmoja kwenye nyanya zilizosindikwa zinazotoka nje.
Pia alisema Serikali imefanya marekebisho nyama kutoka nje ambapo zitatozwa ushuru wa forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 wa zamani kwa mwaka mmoja.