23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Tozo 54 zafutwa, wafugaji kicheko

Ramadhani Hassan-Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema Serikali imefuta tozo 54 zinazotozwa na wizara, idara na taasisi zinazojitegemea ili kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara.

Katika kutekeleza hatua hiyo, alisema katika Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), anapendekeza kufuta tozo za kushikilia usajili wa dawa za chanjo inayotozwa kwa Dola za Marekani 150 (Sh 350,000)  dawa za mitishamba Dola 100 (Sh 230,000) , vitendanishi Dola 250 ( Sh 580,000) chakula Dola 100(230,000), vipukusi Sh. 100,000 na tozo za bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.

Dk. Mpango alisema pia anapendeza kufuta tozo za kudurufu cheti cha usajili wa vitendanishi inayotozwa kwa kiasi cha Dola 100, tozo ya ukaguzi wa maduka mapya ya kuuzia vyakula Sh. 50,000, tozo ya usajili wa maduka ya rejereja ya dawa za mifugo ambayo ni kati ya Sh. 50,000 na 100,000.

Katika mamlaka hiyo, Dk, Mpango pia alisema anapendekeza kufuta tozo ya ukaguzi wa viwanda vya samaki iliyokuwa inatozwa kati ya Sh. 200,000 na 250,000, tozo ya ukaguzi wa maduka mapya ya samaki Sh. 50,000 na tozo ya leseni ya mwaka ya biashara kati ya Sh. 50,000 hadi Sh. 300,000.

Alisema hatua hiyo iliyolenga kuweka mazingira rafiki ya kibiashara na uwekezaji, inatarajiwa kupunguza mapato ya serikali kwa Sh. bilioni 2.5.

Kuhusu tozo za Shirika la Viwango (TBS), Dk. Mpango alisema anapendekeza kufuta tozo ya Sh. 50,000 ya maombi ya alama ya ubora, tozo ya nembo ya ubora ambayo ni asilimia 10 na 15 ya tozo ya gharama za mwanzo za ukaguzi wa ubora, tozo ya dhamana ya cheti cha kutumia nembo ya ubora na tozo ya asilimia 50 ya ununuzi wa fomu ya maombi ya bidhaa zinazotoka nje kwa bidhaa zote.

Tozo zingine zinazopendekezwa kufutwa katika shirika hilo ni za gharama za ugenzi ambazo hutozwa kulingana na umbali wa sehemu (mfano Dar es Salaam umbali wa Km tano ni Sh. 10,000) na tozo ya asilimia 0.2 ya gharama za mzigo na usafirishaji ya udhibiti wa vipodozi, vifaa tiba ikiwa ni pamoja na kondomu, mabomba ya sindano, glavu, pamba na bandeji.

Alisema hatua hiyo inayolenga kupunguza mzigo kwa wafanyabiashara, inatarajiwa kupunguza mapato ya serikali kwa Sh. bilioni 2.687.

Akizungumzia tozo za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Mpango alisema anapendekeza kufuta tozo ya huduma za kusitisha kutoa kibali cha awali na kutoa kibali kipya inayotozwa kwa kiwango cha Dola 50 na tozo ya huduma ya kubadilisha taarifa za kibali inayotozwa kwa kiwango cha Dola 50.

Pia, anapendekeza kufuta tozo ya Dola 500 kwa ajili ya usajili wa kampuni ya Wakala wa Forodha kipindi cha usajili na kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili kwa wasambazaji wakubwa Dola 1,000 na wasambazaji wa kati Dola 500 kwa mwaka.

Aidha, Serikali imependekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Majumbani na Viwandani Sura 182 ambapo marekebisho yake yatahusisha  kutoza tozo ya Sh. 40,000 ya usajili wa kemikali kwa kila kemikali kwa kipindi cha usajili badala ya dola 20.

Pia kutoza kodi ya Sh. 200,000 kwa wafanyabiashara wakubwa na Sh. 50.000 kwa wajasiliamali wadogo kwa kila cheti cha usajili.

Zaidi amependekeza tozo ya Sh. 200,000 badala ya dola 100 kwa wafanyabiashara wakubwa na Sh. 50,000 kwa wafanyabiashara wadogo kwa usajili wa eneo la kuhifadhia kemikali.

Dk. Mpango alibainisha pendekezo la kutoza kodi ya Sh. 300,000 kwa siku kwa kila mtu ya kuchambua kemikali chakavu badala ya dola 300 (Sh 690,000).

“Kutoza tozo ya Sh. 200,000 ya kuanisha na kuidhinisha njia ya kuteketeza kemikali badala ya dola 500,” alieleza.

Kadhalika, serikali imependekeza kutoza tozo ya Sh. 300,000 kwa kila siku kwa mtu ya kusimamia kupakia, kusafirisha, kushusha na kuteketeza kemikali chakavu badala ya dola 300.

Aidha, kutoza tozo ya Sh. 300,000 ya ukaguzi wa maghala na sehemu za kuhifadhia kemikali badala ya dola 200.

Pia kutoza tozo ya Sh. 150,000 kwa kila siku kwa kila mtu kwa tathimini ya njia za usafirishaji na ukaguzi wa dharura badala ya dola 100.

Alisema kwenye mabadiliko hayo ya sheria, serikali imependekeza kutoza tozo ya Sh. 150,000 kwa siku kwa kila mtu kwa kusindika kemikali hatarishi badala ya dola 100.

Alisema ili kutimiza matakwa ya sheria ya kutumia fedha za Kitanzania, tozo zote zilizokuwa zinatozwa kwa dola, hivyo zitatozwa kwa fedha za Kitanzania isipokuwa shehena za kemikali zinazosafirishwa nje ya nchi.

Dk. Mpango alisema hatua hiyo inatarajiwa kupunguza mapato ya serikali kwa Sh. milioni 450.

TOZO 16 MIFUGO ZAFUTWA 

Alisema Serikali imependekeza kufuta tozo mbalimbali kwenye sekta ya mifugo ikiwamo tozo ya Sh. 5000 ya vibali vya vyombo vya kusafirisha maziwa chini ya lita 51.

Pia kufuta tozo ya Sh. 50,000 ya usajili wa vituo vya kukusanyia maziwa lita 201 kwa siku, tozo ya Sh. 5000 ya usajili wa wazalishaji wa maziwa chini ya lita 51 kwa siku na kufuta tozo ya Sh. 500,000 ya usajili wa wasambazaji wa pembejeo za maziwa.

Tozo nyingine iliyofutwa ni ya Sh. 15,000 ya usajili wafugaji wadogo wa mifugo ya nyama na kufuta tozo ya Sh. 50,000 ya usajili wa wafugaji wadogo wa mifugo ya nyama.

Kufuta tozo ya Sh. 50,000 ya usajili wa wafugaji wa kati wa mifugo ya nyama, kufuta tozo ya Sh. 75,000 ya usajili wafugaji wakubwa wa mifugo ya nyama na kufuta tozo ya Sh. 20,000 ya usajili wasimamiziwa minada ya awali.

Alisema Serikali imependekeza kufuta tozo ya Sh. 30,000 ya usajili wasimamizi wa minada ya upili na mipakani pamoja na kufuta tozo ya Sh. 50,000 ya usajili wa minada ya upili na mpakani.

Vilevile, kufuta tozo ya Sh. 30,000 ya usajili wafanyabiashara wa minada ya awali na kufuta tozo ya Sh. 60,000 ya usajili wafanyabiashara wa minada ya upili na mipakani.

Aidha, alisema kufuta tozo ya Sh. 100,000 ya usajili wa wafanyabiashara wa nyama na bidhaa zake za nje ya nchi pamoja na kufuta tozo ya Sh. 1000 ya kibali cha kusafirisha kuku nchini ya vifaranga 100 kwa siku.

Pia alipendekeza kufuta tozo ya sh. 200 ya kibali cha kusafirisha kuku mkubwa nchini.

Dk. Mpango alibainisha hatua hiyo inatarajiwa kupunguza mapato ya serikali kwa Sh. bilioni 16.6.

MARUFUKU TRA KUFUNGA BIASHARA

Aidha Dk. Mpango alisema bajeti hii inakusudia kuimarisha zaidi ufuatiliaji na tathmini  ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi zote. 

Alisema Serikali itaimarisha usimamizi wa ukusanyaji mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa bajeti lakini wakati huohuo kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa kodi unafanyika bila kuathiri biashara.

“Napenda kuwasisitiza tena watumishi wa TRA kwamba hairuhusiwi kufunga biashara ili kushinikiza mfanyabiashara alipe kodi au malimbikizo ya kodi isipokuwa kwa kibali cha Kamishina Mkuu wa TRA”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles