Na RAMADHANI MASENGA
NIAJE wanangu? Mambo ni nini? Masela mwanenu bado buku tu niwe milionea. Hamuamini? Shauri zenu. Niungieni buku mwanenu niwe tajiri namba tatu Tanzania.
Hakika laifu ni mikakati. Bila mikakati na mipango makini hutoboi. Saa mwananenu naelekea kutoboa. Kila mmoja wenu akinichangia buku nami nakuwa milionea.
Nimepigika sana na laifu la Kibongo. Nimesuka sana mipango. Nimekesha nikitafuta mbinu za kitajiri. Sasa baada ya kuhangaika kwa mingomingo nimepata siri. Buku tu itanifanya niwe tajiri namba tatu Tanzania.
Masela nichangieni. Bila kusaidiana hii laifu hatutoboi. Inatajwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya uchumi wa Tanzania unashikiliwa na watu wenye asilia ya kiasia (hasa hawa akina vevee).
Cha kushangaza hawa watu wako asilimia kama 20 tu katika taifa letu. Unajua siri ya kutoboa kwao? Kusaidiana. Hawa watu wanabebana kinoma noma.
Wakimuona mwenzao kakwama, lazima wampige tafu. Sasa wanangu katika mambo mukide kama haya kuigana lazima.
Kama akina cholicholi wanavyopigana tafu, basi msiache kunipiga tafu na mimi mwanenu wa faida. Nichangieni buku niwe milionea masela.
Nimepigika sana katika hili laifu. Nimepata visenti kadhaa nikaishia kuhonga na kubeti. Nimetumikishwa miaka kibao bila mafanikio ya maana.
Kwa siri hii, sitakuwa mtumwa tena wanangu. Nipeni buku nipate utajiri. Kwa miaka zaidi ya kumi nilidhani ili niwe na mijihela ni lazima nirithi mabasi au visima vya mafuta kama watoto wa Kiarabu.
Kwa fikra hizo, kila senti yangu ikaishia kwenye bata na pochi za mademu kwa sababu niliona haitoshi. Sasa nimegundua uchawi wa maisha yangu ni nini.
Mkiniongezea buku tu na mimi natusua. Nakuwa mzito, bosi, milionea. Kila demu aliyenitosa atanifuata na kutaka upya namba yangu ya simu.
Mnajiuliza ni kwanini buku? Basi ngoja niwachane. Kila safari ndefu huanza na hatua chache. Ili ufikie milioni mia, basi unatakiwa uwe na nidhamu ya kutunza pesa ndogo unayopata.
Kwa maana hiyo, ukiwa na uwezo wa kuifanya buku kuwa buku tano ama kumi, basi una uweo wa kuifanya buku kumi kuwa laki. Kwa mtindo huo unaukaribia umilionea bila tabu.
Umegundua nini hapo? Acha uboya. Usilalamike kuwa laifu ni taiti wakati huna nidhamu ya fedha. Unanunua sigara ngapi kwa siku?
Pakti mbili kisha baadaye unalalamika huna hela ya kula. Unatumia kiasi gani kwenye ulabu? Halafu kesho yake unalalama maisha magumu! Oya vipi mwanangu? Acha kuzingua pimbi wewe.
Nishakisanua asa utaamua mwenyewe kujiongeza au uendelee kumbwela. Wenzio tushaachana na mambo ya kupiga vizinga, tunameki ndogondogo daadeki. Nduki kwa sana!