25 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Baba yake wakili wa Zitto afunguka

Albert Msando
Wakili wa Zitto Kabwe, Albert Msando

Na Fadhili Athumani, Moshi

BABA mzazi wa Wakili Albert Msando, anayemtetea Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, Gasper Msando, ameibuka na kudai kuna njama za kumnyamazisha na kumuua mwanaye kisiasa.

Kauli hiyo ya Mzee Msando imekuja siku chache baada ya Idara ya Uhamiaji mkoani Kilimanjaro kumhoji Wakili Msando baada ya kudaiwa si raia wa Tanzania.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatatu Moshi Vijijini hivi karibuni, alisema binafsi anashangazwa na taarifa zinazosambaa kwamba mtoto wake si raia huku akisisitiza kuwa ni Mtanzania halisi kutoka kabila la Kichaga alilorithi kutoka kwake.

Wakili Msando ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mabogini (Chadema), anamtetea Zitto katika kesi yake dhidi ya uongozi wa Chadema katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, akipinga uanachama wake kujadiliwa na Kamati Kuu ya chama hicho.

Alisema tuhuma hizo ni jitihada za watu wachache wanaojaribu kumzima mwanaye huyo kisiasa kutokana na kitendo cha mwanasheria huyo kuwabwaga viongozi wa Chadema mahakamani katika pingamizi lililowasilishwa na Zitto ambalo liliwakera wengi.

“Nashangaa kwanini haya yanaibuka sasa hivi, mimi ni Mchaga, nimezaliwa Kibosho nimekulia Kibosho, watoto wangu wote wamezaliwa nchi hii, iweje leo Albert aambiwe sio raia? Kuna watu hawakuridhika baada ya kesi ile, wanataka kumuua kisiasa,” alisema Mzee Msando.

Mzee Msando ambaye ni dereva mstaafu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), alisema inashangaza kusikia tuhuma hizo dhidi ya mwanaye na kuhoji kama Wakili Msando si raia wa Tanzania uraia wake uko wapi wakati amezaliwa katika Hospitali ya Serikali.

Alisema kwa mara kadhaa tangu mwanaye ahojiwe na Idara ya Uhamiaji amejaribu kumshauri aachane na siasa bila mafanikio.

“Nimejaribu kila mara kumshawishi Msando aache siasa lakini amekuwa mgumu kunielewa, wakati mwingine huwa naonyesha kukubaliana na wazo langu,” alisema Mzee Msando.

Katika hatua nyingine, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Johaness Msumule, alikiri kuhojiwa kwa Msando ingawa alikataa kulizungumzia suala hilo kwa undani akidai lipo katika uchunguzi wa awali.

“Siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa kwa sababu bado ni bichi, nitafute wakati mwingine,” alisema Msumule.

Juni 26, mwaka huu, Wakili Msando, alipeleka maelezo yake katika ofisi ya Uhamiaji mkoani Kilimanjaro baada ya kudaiwa si raia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles