Yohana Paul -Mara
DUNIA imekwisha! Ndilo neno ambalo unaweza kusema baada ya mkazi wa Kijiji cha Balili, Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Meshack Michael kudaiwa kuwabaka binti zake watatu wa kuwazaa kwa miaka kadhaa sasa.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa za tukio hilo jana, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili alilaani na kusema ni ukatili wa hali ya juu ambao kamwe haupaswi kufumbiwa macho.
Alisema mama mzazi wa binti hao ambao ni waathirika, anatakiwa akamatwe ili ahojiwe kutokana na kuficha ukweli wa tukio hilo kwa kisingizio cha kukwepa aibu.
“Kitendo kilichofanywa na baba huyu ni ukatili wa hali ya juu, nimeagiza mama mzazi akamatwe kwa kuhusika na tukio hili kutokana na kuficha taarifa za kubakwa kwa binti zake na kumsingizia mtu mwingine huku akijua ukweli wote.
“Ifike hatua jamii itambue haki za watoto, maana haiwezekani mbali na jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na mashirika ya kupigania haki, bado kuna watu wameendeleza vitendo hivi, haiwezekani kila aina ya ukatili afanyiwe mtoto, jamani inakera na haikubali,” alisema Bupilipili.
Mama mzazi wa binti hao, Gaudensia Meshack alisema tukio la kubakwa watoto wake lilianza kufichuka baada ya mtoto wake wa darasa la tano, Suzan Michael kubainika ana ujauzito.
Alisema baada ya kumhoji kwa lengo la kumtambua mhusika wa ujauzito huo, alimtaja kijana mmoja wa mtaani hapo ajulikanaye kwa jina moja la Msukuma, huku pia akimtaja baba yake mzazi jambo ambalo hakuamini.
Mama huyo alisema akiwa bado anatafakari iliwezekana vipi, ndipo mtoto wa tatu jina linahifadhiwa (mwanafunzi wa darasa la nne) naye alibainika amebakwa alipoenda kuchota maji na kumpeleka hospitalini bila kujua mhusika.
Alisema mchezo mchafu wa mume wake kuendelea kuwabaka wanawe, uliendelea hadi siku alipowafumania wakiwa wamelala na wanashiriki tendo la ndoa kitandani.
“Sikuamini macho yangu baada ya kuingia chumbani na kukuta mume wangu akiwa na mwanangu ambaye kwa sasa ni mke mwenza wakivunja amri ya sita, mume wangu alionekana kuganda kama kapigwa shoti, huku mwanangu akilala kifudifudi kuficha uso wake.
“Nilimuuliza swali mume wangu, umekosa wanawake kote huko hadi uje ulale na mwanao kweli, aliniomba msamaha na kwa kuwa na mimi ni mtu wa Mungu nilimsamehe,” alisema mama huyo ambaye hata hivyo alipaza sauti kuomba Serikali imchukulie hatua kali za kisheria mume wake.
Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto la Kivulini ambao ndio walioibua tukio hilo, Yassin Ally, alisema baada ya uchunguzi walibaini nyuma ya nyumba ya baba huyo alikuwa amejenga kama chumba cha kufanyia unyama huo.
Ally alisema binti wa kwanza ambaye alianza kumbaka kutoka darasa la pili, tayari ameolewa, lakini hadi sasa alikuwa akiendelea kumfanyia kitendo hicho.