27.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

BAADA YA KUMALIZA MADAWATI, SASA ZAMU YA MAABARA

Na Willbroad Mathias


WAKATI  Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, moja ya kazi iliyorithi toka kwa awamu iliyomalizika ni kukabiliana na changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu.

Kutokana na changamoto hizo, Rais John Magufuli aliagiza watendaji serikalini na kuwaomba wadau wa maendeleo kuhakikisha tatizo la upungufu wa madawati linamalizika katika shule za Serikali.

 

Baada ya kauli hiyo, walijitokeza wadau mbambali kuchangia madawati ili kuhakikisha wanafunzi wanaondokana na adha  ya kukaa chini ama juu ya matofari.

Miongoni mwa wadau waliojitokeza kuitikia wito wa  Rais Magufuli ni Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania ambapo kwa nyakati tofauti  wakiongozwa na Balozi Jaseem Al Najeem walitoa misaada ya madawati na kuamsha hamasa kwa wadau wengine wa ndani na nje ya nchi kuchangia. Kazi hiyo ilifanikiwa kwa asilimia 100.

Jitihada, usimamizi na ushirikiano wenye uwajibikaji wa hali ya juu, umezibadili shule nyingi za msingi na sekondari zinazomilikiwa na serikali kuondokana na  hali ya watoto kukaa chini kwa kukosa madawati.

Baada ya kufanikiwa kwa kazi hiyo, kwa sasa jitihada zimeendelea kufanywa na viongozi  wa ngazi mbalimbali ili kuhakikisha upungufu wa vyumba vya madarasa nao unamalizwa, hasa ukizingatia kuwa hali iliyopo katika shule za serikali ni kwamba madawati ni mengi ukilinganisha na vyumba vya madarasa vilivyopo.

Pia juhudi zilikwisha anza za kuhakikisha kila shule ya sekondari inakamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara kwa ajili ya kufundishia masomo ya Sayansi.

Kutokana na jitihada hizo, pia Serikali ya Kuwait kupitia Balozi wake hapa nchini, Al Najem haikuchoka kufuatilia matatizo shuleni kutokana na kutambua kwamba shule zenye mazingira bora ndizo zinazowajenga vijana wenye kumudu mazingira ya kisasa na kuendeleza nchi kwa misingi ya teknolojia za kisasa na kuisukuma kwenye uchumi wa kati.

Hatua ya Balozi  Al Najem kujitosa katika vita hiyo ilikuja baada ya  kutangazwa matokeo ya kitado cha nne mwaka 2016 ambapo serikali ya Kuwait ilifuatilia na  kugundua masomo ya Sayansi na Hisabati yameendelea kutoa matokeo mabaya si kwa wanafunzi wa shule za umma bali hata zile za binafsi kutokana na shule nyingi kukosa maabara za kufundishia masomo hayo.

Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Cordoba iliyopo Msasani kwa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam ni moja kati ya shule ambazo zimenufaika na msaada huo wa Serikali ya Kuwait, baada ya kupewa vifaa vya maabara kwa ajili ya kufundishia masomo ya Sayansi.

Akikabidhi msaada huo hivi karibuni wenye thamani ya dola milioni saba Balozi Al Najem anasema kuwa kazi hiyo itakuwa ni ya kudumu  na kwamba watazifikia shule za umma nchi nzima.

“Nina imani iwapo tutaunganisha nguvu kama zile za kwenye madawati na kuendelea kuhamasisha asasi za kiraia, balozi na wadau wa maendeleo kuchangia kampeni hii ya yenye lengo la kuboresha mazingira bora ya watoto kujifunza ili kuongeza viwango vya ufaulu na  kujitegemea kwa nguvukazi yenye ujuzi itakayosukuma maendeleo,” anasema balozi huyo.

Anasema umuhimu wa maabara za sayansi na kompyuta shuleni huwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kupata uzoefu mpya kuliko kusoma kinadharia tu.

Balozi Al Najem anasema maabara ni chimbuko la kuwafanya wanafunzi kujifunza, kujenga tafakuri na umakini. Pia huleta ushindani, ugunduzi na ubunifu miongoni mwa wanafunzi.

“Kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa zinaonesha kuwa shule zenye maabara zilizosheheni vifaa vya kisasa huwawezesha walimu kutoa wanafunzi wenye uwezo mkubwa wa kutafsiri mambo, pia walimu nao hufanya kazi zao kwa ufanisi na muda wote wanafunzi huwa  na ari ya kujifunza kwa bidii zaidi kwa vitendo,” anasema balozi huyo.

Balozi Al Najem anasema hakuna namna nyingine ya kulikwamua Taifa bila  kunyanyua viwango vya elimu na kukamilisha ujenzi wa maabara na upatikanaji wa vifaa vya kufundisha sayansi. Anasema maendeleo makubwa ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali katika kila sekta mafanikio yake yanategemea zaidi Sayansi na Teknolijia.

Anasema wanapopatikana wahisani inabidi kuwaunga mkono na kushirikiana nao  ili kuweza kutatua janga hilo la ukosefu wa maabara kama ilivyokuwa kwa upande wa madawati.

“Kufanya hivyo ndani ya kipindi kifupi tutazalisha nguvu kazi yenye ujuzi itakayobadili sekta za kilimo, ufugaji uhandisi, udaktari, biashara, ujenzi na mawasiliano zenye matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia,” anasema Balozi Al Najem.

Anasema hakuna nchi duniani iliyoweza kupiga hatua ya maendeleo bila kuwa na wataalamu wa kutosha kwenye masomo ya Sayansi, ndiyo maana Serikali ya nchi yake imekuwa mstari wa mbele kuchangia sekta ya elimu ili iweze kutoa elimu bora kwenye mazingira bora na vijana waweze kuandaliwa vyema na kuwa nguvu kazi yenye ujuzi siku zijazo.

Balozi Al Najeem anahimiza kwamba ni lazima upatikanaji wa vifaa katika maabara ya kufundishia masomo ya Sayansi kwa kile anachodai ni kuunga mkono kauli aliyowahi kuitoa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa akisisitiza  kuwa shule yoyote ya sekondari ni ile yenye walimu, vitabu  na maabara za masomo ya sayansi kwani zinatoa fursa na nafasi ya kujenga udadisi wa wanafunzi  ari ya kujifunza na kujiamini kwani hawatakuwa na woga wa kuthubutu.

“Tanzania kama yalivyo mataifa mengi ya Kiafrika imekuwa ikikabiliwa na  tatizo la kutokuwa na wataalamu wengi wa masomo ya uhandisi, madaktari na wanasayansi wa fani mbalimbali kutokana na wahitimu wa vyuo na shule kushindwa kutafsiri mambo waliyojifunza kwa nadharia kwenda kwenye vitendo,” anasema balozi huyo.

Balozi Al Najeem anasema uwepo wa maabara za kutosha utawajengea pia wanafunzi uwezo wa kufanya tafiti na kukusanya takwimu sahihi ili kupata matokeo yenye uhakika.

Anasema ni muhimu tukaunga mkono ushauri na jitihada za shule na vyuo vyetu kuwa na maabara za kisasa kwani masomo ya Sayansi ni tofauti na masomo mengine kutokana na kwamba ili  kuyaelewa kufanya  matendo ya kushika kuona na kuonja kwa kutumia milango mitano ya fahamu ili kujenga taifa la wadadisi na wachunguzi.

 

Serikali yagawa vifaa vya maabara

Pamoja na jitihada zinazofanywa na watu wa mataifa ya nje, kuisaidia Tanzania katika kuboresha sekta ya elimu, wiki iliyopita Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi ilipokea vifaa vya maabara ya masomo ya Fizikia, Kemia na Baolojia vyenye thamani ya Sh bilioni 16.9 kwa ajili ya shule za sekondari nchini.

Vifaa hivyo vilitolewa na Kampuni ya Lab Equip Ltd ambayo ni miongoni mwa wazabuni watano walioshinda kusambaza vifaa hivyo kwa kanda 11 ambazo ni Kaskazini Mashariki na Kaskazini Magharibi.

Nyingine ni Kanda za Magharibi, Kati, Kusini, Ziwa, Nyanda za Juu, Dar es Salaam, Mashariki, Ziwa Magharibi na Nyanda za Juu Kusini.

Msaada huo ulipokelewa na Kaimu Kamishna wa Elimu wizarani hapo, Nicolas Buretta aambapo alisema vifaa hivyo vitasambazwa katika shule 1,696 za sekondari  nchini.

Alisema kuwa kati ya hizo, shule 1,625 ni za kata na shule 71 ni shule kongwe za Serikali.

Alibainisha kuwa vifaa hivyo vitasambazwa katika shule zilizokamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara na kwamba, hiyo ni changamoto kwa shule ambazo hazijakamilisha majengo yao ili zikamilishe.

Alisema; “vifaa hivyo vitasambazwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ)… kazi hiyo ya usambazaji itakamilika mwishoni mwa mwezi huu.

“Tunaamini kuwa vifaa hivi vitaleta matokeo chanya katika masomo ya Sayansi. “Pia utainua ari kwa wanafunzi katika kujifunza kwani wataanza kusoma kwa vitendo badala ya nadharia. “Hii pia itasaidia kulifanya Taifa kuwa na wataalamu wa kutosha kwa kuwa hatutakuwa na changamoto ya vifaa vya maabara,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni ya Lab Equip Ltd, Hassan Raza anaishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuwaamini na kuwapa jukumu hilo, ambalo wamelifanya kwa umakini wa hali ya juu.

 

Hali ilivyo shuleni

Shule nyingi hasa za kata hapa nchini zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa vya maabara, walimu hasa wa Sayansi na vitabu vya kufundishia.

Licha ya kukosa vifaa, nyingine hazina kabisa hazina maabara ya kufundishia kwa
vitendo masomo ya Sayansi.

Wanafunzi wanaosoma katika baadhi ya shule za kata wanasema kuwa tangu waanze kidato cha kwanza mwaka huu hawajawahi kuingia maabara.

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Lumo, ambaye hakupenda jina lake liwekwe gazetini anasema kuwa tangu aanze kidato cha kwanza mwaka huu shuleni hapo, hajawahi kujifunza kwa vitendo na hajui kama shule hiyo ina maabara ya kujifunzia.

Suala hili linadhihirisha wazi kuwa suala la maabara katika shule za kata ni kama anasa, mwanafunzi anapojifunza darasani huwa hakuna kawaida ya kwenda kufanya majaribio kwa vitendo.

Katika shule nyingine, walimu wa Sayansi hakuna hivyo wanafunzi huwalazimu kusoma masomo mengine hata yale ambayo hawayapendi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles