28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

KUTANA NA ‘BWANA MLA VYOTE’

Alikula ndege, baiskeli 18


KUNA kila aina ya watu wa ajabu duniani, lakini jamaa huyu- Michel Lotito anaonekana kushika nafasi ya juu zaidi miongoni mwa watu hao.

Kwa vile alikuwa na mlo wa ajabu, alipenda kula vyuma usiku na mchana na alivitamani kweli kweli.

Alifurahia mlo wa seti ya televisheni na baiskeli, misumari na balbu. Kadiri unavyomtajia vitu vingine ambavyo si chakula cha binadamu, hamu ya kuvila humjia.

Kwa sababu hiyo, anajulikana kama ‘Monsieur Mangetout’ Kifaransa chenye maana ya Bwana Mla Vyote” au ‘Bwana Mla Kila Kitu’.

Hakika si utani, mkazi huyu wa Grenoble nchini Ufaransa, ana uwezo wa kula kila kitu kuanzia baiskeli ikiwamo spoku zake hadi ndege nzima aina ya Cessna 150 na mashine yake.

Kati ya mwaka 1959 na 1997 inakadiriwa alikula tani tisa ya vyuma.

Bila shaka wakati ukisoma makala haya, utajiwa na mawazo, inawezekanaje kwa mtu kula vyuma na glasi? Hakika ni kitu ambacho hakiwezi kuingia akilini mwako kukiamini kwa vile ulaji huo husababisha madhara makubwa ya afya.

Lakini ukweli ni kwamba uwezo wake huo ulitokana na kuugua hali ijulikanayo kwa kitaalamu kama Pica, ambayo husababisha mtu kuwa na uchu wa kula vitu kama uchafu, glasi, mipira na hata chuma aina yoyote.

Ni ulaji ambao ungeweza kufikiria unaweza kusababisha kuziba kwa utumbo na kufanyiwa upasuaji wa dharura kwa watu wa kawaida na au kusababisha sumu hatarishi kwa maisha yake achilia mbali mlolongo mwingine wa matatizo ya kiafya.

Bahati nzuri mno kwake, mburudishaji huyo ana kile, ambacho madaktari walikieleza kuwa na tumbo na utumbo wenye ngozi nene.

Mfumo huo umewezesha vitu vikali kama chuma kupita tumboni katika mfumo wake bila kusababisha athari zozote za kiafya wala muundo au mfumo wa utumbo wake.

Mbali ya vyuma na vitu vingine, sumu kutokana na vitu hivyo hazikuonekana kumsababishia matatizo yoyote ya kiafya.

Lotito alijigundua kuwa ana uwezo huo kwa mara ya kwanza wakati glasi ambayo alikuwa akinywea kinywaji, ilipovunjika na kujikuta akitafuna vipande vya glasi hiyo.

Alikuwa muumini wa dozi ndogo ndogo, kwa kuvunja au kukata kata vipande vidogo na kuvila kwa maji mengi.

Katika kufanikisha hilo ipasavyo, aliweza kunywa kiwango fulani cha mafuta yenye madini ili kusaidia kuviongoza vipande vya vyuma kuelekea katika mfumo wake wa utumbo.

Aliweka ukomo wa mlo wa vyuma kwa kilo moja kwa siku. Alimeza baiskeli 18 na ilimchukua miaka miwili kumaliza kula ndege.

Tukio la kula ndege alilihesabu kama karamu kubwa zaidi katika maisha yake, aliikata kata na hakubakiza kitu ikiwamo mashine, ambayo nayo iliingia tumboni mwa Bwana huyu Mla Kila Kitu.

Lotito pia alikula vigari 15 vya kuwekea vitu vya manunuzi katika maduka ya kisasa, seti saba za televisheni, vifaa viwili vya kutelezea katika barafu, taa sita aina ya chandeliers, vitanda viwili, jeneza, kompyuta na kipande kidogo cha mnara maarufu wa Eiffel uliopo jijini Paris.

Ajabu zaidi, hupata shida kula na kumeza ndizi na mayai ya kuchemsha.

Kilele zaidi cha mafanikio yake kilikuja mwaka 1981, kuthibitisha kuwa alikuwa na uwezo kuliko mashine.

Siku moja Lotito alishambuliwa na kuchomwa visu kikatili na kumsababishia majeraha ya kutishia maisha.

Alikutana na upasuaji mchungu hadi uponaji wenye kuleta maumivu kutokana na masharti yaliyoambatana nao.

Baada ya tukio hilo akaenda kulila roboti zima kidogo kidogo na kulimaliza wiki tatu baadaye.

Wataalamu na wachambuzi wa masuala ya roboti hasa wanaofuatilia hofu iliyopo kwamba ipo siku mashine hizo za kielektroniki zenye akili ya kibinadamu zitakuja kuwa tishio kwa binadamu, wana haya ya kusema:

“Kutokana na uwapo wa tishio la uwezekano wa roboti kuzua vuguvugu la upinzani dhidi ya binadamu, Lotito angekuwa mtu sahihi wa kukabiliana na tishio hilo. “Inasikitisha ameondoka kabla ya tishio hilo kuwa kweli.” Wanasema.

Ni kwa sababu Lotito alifariki dunia Juni 2007, muda mfupi baada ya kutimiza siku yake ya 57 ya kuzaliwa. Inasemekana alifariki dunia kwa sababu za kawaida.

Sawa hebu fikiria tani tisa za chuma zilizopita katika mfumo wake wa mmeng’enyo wa chakula, bado eti hazihusiani na kifo chake!. Ajabu kiasi gani?

Tisa kumi, Mfaransa huyo mwenye hamu kubwa ya kula vitu kama ndege, ana mfumo wa mmeng’enyo wa chakula usioweza kuhimili mayai ya kuchemsha! Ajabu iliooje.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles