23.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Azam yailainishia ubingwa Yanga

pic+azam*Mambo ya Leicester City huenda yakatokea Bongo

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

UAMUZI wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TFF) kuipoka ushindi wa pointi tatu na mabao matatu klabu ya soka ya Azam katika mchezo wake dhidi ya Mbeya City uliochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, umeonekana kulainisha mbio za ubingwa kwa timu ya Yanga ambayo itakuwa ikisubiri pointi tatu ili kutangazwa kuwa mabingwa msimu huu.

Lakini pia, Yanga inaweza kutangaza ubingwa kama timu ya Leicester City ya England, iliyotangaza ubingwa huo kupitia matokeo ya sare ya bao 2-2 katika mchezo kati ya timu ya Chelsea na Tottenham Hotspur uliochezwa Uwanja wa Stamford Bridge jijini London, Jumatatu kwani mchezo wa Jumapili kati ya Simba na Mwadui FC unaweza kuamua bingwa wa Ligi Kuu Bara.

Azam ilipokonywa ushindi huo  katika mchezo  namba 156, ambao iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 ulioongeza kasi ya ushindani wa ligi hiyo.

Hatua hiyo inaifanya Yanga kuendelea kuwa kileleni kwa pointi 68 na Azam kushuka nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 57 zote zikiwa zimebakiwa na michezo mitatu mkononi, huku Simba ikipanda hadi nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 58 ikiwa na mchezo minne mkononi.

Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ kwa vyombo vya habari, ilisema kuwa uamuzi huo ulitokana na timu hiyo kumtumia mchezaji, Erasto Nyoni, kwenye mchezo huo wakati akiwa na kadi tatu za njano.

“Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 37(4) ya Ligi Kuu Toleo la 2015 inayoelekeza kuwa mchezaji atakayeonywa kwa kadi ya njano katika michezo mitatu, hataruhusiwa kucheza mchezo unaofuata wa timu yake hivyo kwenda kinyume na januni husika,” ilisema taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo ilisema kuwa uamuzi huo ulizingatia Kanuni ya 14 (37) ya Ligi Kuu Toleo la 2015, ambapo timu ya Mbeya City itafaidika kwa kupewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.

Bodi hiyo imelionya benchi la ufundi la timu hiyo kuongeza umakini katika utunzaji wa kumbukumbu za kadi za wachezaji wake na kuzikaribisha timu zote wakati wowote kuomba kumbukumbu zozote kila zinapohitajika.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba, alisema wameipokea barua hiyo ya TFF na wataifanyia kazi.

“Tumepokea barua ila haijaeleza mchezaji alipata kadi katika mechi zipi, tutajiridhisha na sisi tutatoa taarifa baadaye,” alisema Kawemba.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara, alisema bado hesabu za ubingwa hazitoi mwanya wa timu yoyote kujitangaza kabla  ligi haijamalizika.

“Hakuna aliyetarajia kama Azam itapokonywa pointi tatu, hivyo ni vigumu kufahamu timu gani itaibuka bingwa kwa kuwa michezo ya mwisho ya ligi ndiyo itaamua.

“Sizungumzi kwa sababu tumenufaika na uamuzi huu, bali ni vizuri Shirikisho la Soka Tanzania kuwa na rekodi ili kusaidia klabu ambazo zitakuwa zimepitiwa katika jambo hili, pia itasaidia kuondoa ushindi wa mezani unaopunguza ushindani,” alisema Manara.

Naye Ofisa Habari wa klabu ya soka ya Yanga, Jerry Muro, alisema kupokonywa pointi tatu kwa timu hiyo ni pigo kwa wadau wa soka na timu shindani kwa kuwa imepunguza kasi ya ushindani katika ligi hiyo.

“Mbali ya kutuhakikishia ubingwa ikiwa tofauti na matarajio yetu, kama wadau wa soka tumesikitika kwa kilichowakuta wapinzani wetu katika mbio za ubingwa msimu huu, lakini pia hatusiti kuonyesha furaha yetu kwani imeleta unafuu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles