24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Azam yaifungia kazi Simba, Hall kicheko

azam-1NA MWANDISHI WETU

TIMU ya Azam imewafungia kazi wapinzani wao Simba kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) Jumamosi hii baada ya kupanga programu kali kwa wachezaji wake.

Azam FC ilianzia maandalizi yake ya nguvu mkoani Tanga kwa kambi ya siku tano na kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Mgambo JKT na African Sports, zote zikiisha kwa sare ya bao 1-1 kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam jana.

Katika kujiandaa zaidi na mchezo huo muhimu dhidi ya Simba, leo saa nane mchana timu hiyo inatarajia kuingia kambini rasmi kwenye makao makuu yake Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Ofisa habari wa timu hiyo, Jaffar Idd, alilipasha MTANZANIA jana kuwa timu itakayoingia kambini itawahusisha pia wachezaji waliokuwa timu za Taifa kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji nchini Ethiopia.

“Maandalizi yetu tulianzia Tanga, hivyo kesho (leo) tutaingia kambini kumaliza maandalizi ya mchezo wa Simba, tutaingia kwenye mchezo huo tukiwa kileleni hivyo tumepania kufanya vizuri kwenye mchezo huo ili kuendelea kukaa kileleni,” alisema.

Wachezaji waliokuwa kwenye michuano ya Chalenji ambao wataripoti kwenye mazoezi ya leo jioni baada ya kuingia kambini ni nahodha John Bocco ‘Adebayor’, nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, Shomari Kapombe, Ame Ally ‘Zungu’, Mudathir Yahya, Aishi Manula, Allan Wanga, Didier Kavumbagu, ambao wote hawakuwepo kambini mkoani Tanga.

Akizungumzia kambi ya mkoani Tanga, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alionyesha kufurahishwa nayo akidai imempa nafasi ya kuwasoma wachezaji wake ambao hawakuweza kucheza kwa muda mrefu.

“Mbali na kujua ufiti wa wachezaji wangu kwa mechi za kirafiki mbili tulizocheza, pia nilipata nafasi ya kujaribu mfumo wa 3-4-3 na nikatumia pia mfumo wangu wa kawaida wa 3-5-2,” alisema.

Hall alisema baada ya kikosi chake kuwasili, chote kuanzia leo ataanza kutoa mafunzo ya mbinu kuelekea mchezo wa Simba na alishindwa kufanya hivyo kabla na baada ya kuwakosa nyota wake 12 waliokuwa timu za Taifa.

“Tunajua namna tunavyoenda kucheza na Simba, najua kikosi nitakachokitumia, naamini tutafanya vizuri kwenye mchezo huo kwa kutumia mambo yetu ya kiufundi tuliyojipangia, sisi tuna kikosi bora zaidi na ndio maana hatuhangaiki kusajili hivi sasa,” alisema.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa kileleni kwenye msimamo ikiwa na pointi 25 na mpaka sasa haijafungwa mchezo wowote katika mechi tisa ilizocheza, ikifuatiwa na Yanga iliyojikusanyia 23, Mtibwa Sugar 22 na Simba 21.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles