NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Dylan Kerr, ameanza kujivunia kikosi chake kuwa kwa sasa kipo imara na kinaweza kumpatia matokeo mazuri kwenye mechi zilizobakia za Ligi Kuu Tanzania Bara kama ilivyokuwa mkakati wake.
Simba hivi karibuni ilifanikiwa kuifunga Kimbunga FC ya Zanzibar kwa mabao 5-2, ikiwa ni mchezo wao wa kwanza wa majaribio tangu ligi isimame, kesho itajipima tena na timu nyingine visiwani humo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kerr alisema kadiri siku zinavyokwenda timu yake inazidi kuimarika hivyo kuendelea kumpa matumaini kuwa malengo aliyojiwekea na makubaliano yake na uongozi ya kuifikisha timu nafasi ya pili yatatimia.
“Nina timu nzuri na imara, wachezaji wote wanajitambua na wanatambua majukumu yao, wanajua nini nataka na wanatekeleza yote hata kama kuna mapungufu, basi ni machache,” alisema.
Mwingereza huyo alisema anafurahishwa na kiwango cha kila mchezaji kwenye timu yake kwa sasa, kwani kila mmoja ameweza kuonyesha uwezo wake jambo ambalo analifurahia.
Naye kwa upande wake, ofisa habari wa klabu hiyo, Haji Manara, alisema bado wanaangalia timu watakayojipima nayo kesho ambapo hadi leo timu hiyo itakuwa imefahamika na tayari kwa kucheza nayo.
“Tunachagua timu kulingana na uhitaji wa mwalimu, hivyo kama atahitaji zaidi tutamtafutia lakini kwa sasa amehitaji mechi hizo mbili na tayari moja ameshaipata na hii ya pili watacheza Jumanne (kesho),” alisema.
Simba inayoshika nafasi ya nne kwenye ligi ikiwa na pointi 21, imeweka kambi visiwani humo ikiwa ni mahususi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya vinara Azam FC, utakaofanyika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Jumamosi hii.