UONGOZI wa klabu ya soka ya Azam, umesema kwamba ubora wa klabu hiyo msimu ujao utaimarika mara dufu baada ya kuajiri makocha vijana kuwazidi wapinzani wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao bado wanahaha na makocha wenye umri mkubwa.
Kauli hiyo ya Azam inatokana na hivi karibuni kuajiri makocha wawili vijana kutoka klabu ya Deportivo Tenerife ya Hispania akiwamo Kocha Mkuu, Zeben Hernandez na msaidizi wake, Jonas Garcia, baada ya kuachana na kocha wao wa zamani, Stewart Hall.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Saad Kawemba, alisema klabu zinatakiwa kuendana na mabadiliko ya soka duniani ndio maana wao waliamua kuajiri makocha vijana ili kuendana na kasi iliyopo.
“Ni makocha hodari na imara hawatayumbishwa na jambo lolote, hata hivyo tumeamua kuwa tofauti na klabu nyingine hapa nchini.
“Pia tumeamua suala la usajili liwe chini yao na kuondoa dhana ya lazima usajili ufanywe na viongozi kama ilivyo kwa wapinzani wetu,” alisema Kawemba.
Kawemba aliongeza kwamba ingawa hadi sasa hawajafanya usajili wa aina yoyote hadi pale makocha hao watakapowasili kutoka mapumziko nchini Hispania, hawatishwi na wapinzani wao kwa kuwa hawazingatii utaratibu wa kufanya usajili wenye tija.
“Klabu pinzani zinafanya usajili lakini hauna tija kwa kuwa unafanywa na viongozi badala ya kocha wa timu husika, ndio maana kunakuwa na vitendo vya kuwafukuza makocha mara kwa mara,” alisema Kawemba.
Akimzungumzia Hall, Kawemba alisema kwamba bado angeweza kuwa kocha wa timu hiyo kama angependa kuendelea kukinoa kikosi hicho.
“Hall ni kocha ambaye anajua kila kitu kuhusu Azam FC, ndio maana tunamtumia mara kwa mara tukiona haja ya kufanya hivyo,” alisema Kawemba.