Avelyn Kitomari-Dar es Salaam
ZAIDI ya Asasi za Kiraia (AZAKI) 200 kutoka maeneo yote nchini zimeshiriki kuandaa andiko la namna ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa kukabiliana na janga hilo.
Mratibu wa Kitaifa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema wameandaa mpango huo kwa kufanya tathmini na kuainisha changamoto zilizojitokeza.
“Pia tumeangalia madhara mbalimbali yaliyotokea na kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kuwa sehemu ya kuendeleza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na janga hili.
“Katika mpango mkakati wetu maeneo ambayo AZAKI imepanga kushirikiana na Serikali ni pamoja na uhamasishaji juu ya hatua za kujikinga, utoaji wa huduma,ushauri na kusaidia pale changamoto zinapojitokeza, mikakati ya kupunguza matokeo hasi , pamoja na kuweka mpango wa pamoja baina ya Serikali na sisiI”,alisema.
Aliipongeza Serikali kwa hatua wanazochukuwa kukabiliana na ugonjwa huo na kusema ipo haja ya kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile alisema Serikali itaendelea kushirikiana na AZAKI katika kupambana na maambukizi ya corona.
Alisema AZAKI pamoja na wananchi wanao, wajibu wa kushirikiana na Serikali kupambana na ugonjwa huo, ambao ni janga la dunia lililoleta athari za kiuchumi na kiafya na kusabisha vifo vingi kwa muda mfupi.
Mwenyekiti Shirikisho la Vyama la Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Ummy Nderiananga aliwashukuru wataalamu wa afya kwa huduma wanayoitoa kwa wananchi waliopata maambukizi ya ugonjwa huo.