27 C
Dar es Salaam
Friday, May 27, 2022

Yanga maneno tumeyasikia tunasubiri vitendo

Mwandishi Wetu

BAADA ya miaka mingi kuonekana ni jambo lisilowezekana kutokana na kutumika kama silaha ya kuwaingiza wagombea madarakani wakati wa uchaguzi, klabu ya Simba ilifanikiwa kumiliki uwanja wake wa mazoezi wenye hadhi.

Uwanja huo uliopandwa nyasi bandia, unapatikana eneo la Bunju, pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam.

Kwa mara nyingine MTANZANIA tunachukua fursa hii kuipongeza Klabu ya Simba kwa hatua hiyo kubwa ya kimaendeleo.

Mashabiki wengi wa soka nchini, wa Simba na wasio wa klabu hiyo walikuwa wanaamini suala la kumiliki uwanja wa kisasa litabaki kuwa porojo kama ambavyo wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wamekuwa wakitumia kuwalaghai wapiga kura ili wawaunge mkono na kuwaingiza madarakani.

Ni sahihi tukisema Simba imejikomboa na aibu  ya kujigamba ni klabu kongwe nchini huku ikiwa haina uwanja hata wa mazoezi unaokidhi.

Kilichofanywa na Simba chini ya Mwekezaji wake Mohamed Dewji si  tu kuikomboa klabu hiyo, ni kulikomboza taifa  zima la Tanzania.

Mafanikio iliyofikia Simba sasa katika uwekezaji nje ya uwanja ni mafanikio ya nchi nzima.

Suala la klabu kutakiwa kumiliki viwanja vyake limekuwa likipigiwa kelele na mamlaka inayosimamiwa soka nchini yaani TFF kwa miaka mingi bila mafanikio.

Lakini ili kupata maendeleo ya kweli katika suala kwanza kabisa lazima klabu zimiliki miundombinu yake inayokidhi ambayo makocha hawatapata tabu kufundisha mbinu zao kwa wachezaji.

Bahati nzuri wamiliki wa klabu ya Azam waliliona hilo mapema na kuamua kwa dhati kujenga uwanja wao ambao leo hii unatumiwa na timu yao kwa michezo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Na si Azam pekee, uwanja wa klabu hiyo umekuwa ukitumiwa pia kwa michezo ya timu mbalimbali hususani zinazoshiriki Ligi Kuu kama uwanja wao wa nyumbani.

Na zaidi umekuwa ukitumiwa kwa michezo ya timu za taifa hasa zile za vijana za wanaume na hata timu ya Taifa ya Wanawake.

Ni imani yetu kwamba, hata uwanja wa Simba hautaishia kutumiwa na klabu hiyo pekee, pia utatumiwa na  timu nyingine.

Hakuna asiyejua changamoto ya upungufu wa viwanja inavyolikabili taifa  hili, hivyo kilichofanywa na Simba si kitu kidogo. Ni mchango mkubwa kwa serikali ambayo pekee haiwezi kumaliza changamoto ya upungufu wa viwanja vyenye ubora katika nchi.

Ukweli ni kwamba Simba sasa itaondokana na gharama ilizokuwa inatumia kukodi  viwanja  kwa ajili ya timu kufanyia mazoezi.

Fedha zitakazookolewa kwenye viwanja vya kukodi, zitatumika kufanya shughuli nyingine za uendeshaji wa klabu.

Ni matarajio yetu, klabu nyingine zitaachana na udanganyifu kwamba zinamiliki viwanja wakati ukweli ni kwamba havina hadhi ya kuchezewa mchezo wa soka na badala yake vitafuata nyayo za klabu ya Simba.

Jingine la kujifunza mashabiki wa soka ni kwamba vurugu haziwezi kusaidia klabu zao kupiga hatua ya kimaendeleo zaidi ya utulivu, ambao utawafanya viongozi kukaa chini ya kutafuta njia sahihi za kuondokana na changamoto zilizoko.

Yanga kupitia mdhamini wake Kampuni ya GSM imeweka wazi nia yake ya kuijengea klabu hiyo uwanja wenye hadhi. Tunasubiri kuona hilo likifanyika kwa vitendo kama tulivyoishuudia Simba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,454FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles