TRIPOLI, Libya
MAPIGANO mapya yamezuka kwenye wilaya za kusini za mji mkuu wa nchini hii, Tripoli, wakati mzozo uliochukuwa miaka kadhaa kati ya serikali hasimu ukizidi kupamba moto.
Wakazi wa mjini hapa walisema jana kwamba walisikia milio ya maroketi na risasi katika wilaya kadhaa, ikikisiwa kuwa ni majibizano ya silaha kati ya wanajeshi wa serikali na wale wa mbabe wa vita, Jenerali Khalifa Haftar.
Haftar haitambui serikali ya hapa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na badala yake anaiunga mkono serikali hasimu iliyopo mashariki mwa nchi hii.
Msemaji wa jeshi la serikali, Mustafa al-Mejii, alisema wameanzisha awamu mpya ya mashambulio baada ya kutolewa amri kuwataka wasonge mbele na washikilie maeneo yaliyomo mikononi mwa waasi.
Hata hivyo, wapiganaji wa Haftar walisema wameyashika maeneo mapya kwenye mstari wa mapambano ndani ya mji huu.
Waziri Mkuu wa nchi hii, Â Fayez al-Serra, ameushutumu ukimya wa jumuiya za kimataifa ambao ni washirika wao kuacha kuingilia kati mapigano hayo.
Serra alisema kuwa juzi walifanya mashambulio saba ya anga katika maeneo yanayoshikiliwa na jeshi la wapinzani wao linaloongozwa na Jenerali Haftar (LNA).
Kundi hilo limekuwa likizidi kusonga mbele likitokea maeneo tofauti na inasemekana limeshachukua uwanja wa ndege wa kimataifa uliopo mjini hapa.
Serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa (UN) inasema imezidisha mashambulio ili kuyapunguza nguvu majeshi ya Jenerali Haftar ambaye ni ofisa wa zamani wa jeshi aliyekabidhiwa kuliongoza kundi hilo mwaka 2015.