GURIAN ADOLF -SUMBAWANGA
JESHI la Polisi Mkoa wa Rukwa linawasaka watu wasiofahamika kwa tuhuma za kumwua kwa kumkata mapanga Mandago Mboje (30) mkazi wa Kijiji cha cha Kizi, Kata ya Paramawe,Tarafa ya Namanyere wilayani Nkasi.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Justine Masejo alisema tukio hilo lilitokea usiku wa Mei 26 majira ya saa mbili za usiku mara baada ya watuhumiwa hao kufika nyumbani kwa marehemu.
Kamanda Masejo alisema kuwa kabla ya Mboje kuuawa, watu hao walifika nyumbani kwake na kuomba hifadhi wakidai wao ni wageni katika kijiji hicho wametokea mbali wakitafuta ng’ombe wao waliopotea.
“Hivyo waliomba walale nyumbani kwa marehemu huyo ili kesho yake waendelee na kazi ya kuwatafuta ng’ombe hao katika mazizi yaliyopo kijijini hapo,”alisema.
Aidha kamanda huyo alisema baada ya kupokelewa na marehemu, walipewa chakula cha jioni na kuandaliwa maji ya kuoga na kuonyeshwa sehemu ya kulala.
“Walipoingia chumbani kwa lengo la kulala, baada ya muda mfupi wageni hao waliamka na kwenda kwenye chumba alichokuwa amelala mwenyeji wao na kisha kumvamia na kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Walipohakikisha kuwa amekufa wakatoka ndani ya nyumba hiyo na kuondoka na hawakuweza kukamatwa kwa kuwa majirani hawakuwa na taarifa ya ugeni huo, wala hawakwenda kutoa taarifa katika serikali ya kijiji kuhusu uwepo wa wageni hao kijijini hapo,”alisema kamanda huyo.
Kutokana na hilo, alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa lengo la kuwabaini waliofanya mauaji hayo, ili watakapobainika wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili kuhusiana na tukio hilo.
Aliwaonya mkoa huo, kuacha kuwapokea wageni wasiowafahamu na kuwapa hifadhi bila kushirikisha viongozi wa serikali wa eneo husika, kwa kuwa ni hatari kwao na familia zao kwani baadhi wa wageni wanaweza kuwa majambazi.