31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wanasheria wachambua hukumu ya Zitto

Na FARAJA MASINDE -DAR ES SALAAM

HATMA ya Zitto Kabwe kisiasa baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumtia hatiani kwa kosa la uchochezi, na kuhukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja imechambuliwa na baadhi ya wanasheria ambao baadhi wanaona bado Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania haimzuii kugombea nafasi yeyote lakini pia wapo wanaoona inaweza kutumika kumuharibia njia.

Awali kulikuwa na hofu kwamba pengine hukumu hiyo inaweza kuzuia ndoto ya Zitto kuwania nafasi yeyote ikiwamo ile ya ubunge anayoshikilia sasa na ile ya juu ya kabisa ya urais.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 67 (2) imeeleza sababu nane zinazomnyima mtu sifa ya kuchaguliwa kuwa mbunge kati yake mbili zinamhusu mtu huyo kama amehukumiwa na mahakama.

Vipengele hivyo ni “(c) ikiwa mtu huyo amehukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa muda unaozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu; au (d) Ikiwa katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu amepata kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma”.

Kuhusu sifa za urais Katiba imetamka wazi katika ibara ya 39 (e) ambayo; mtu atachaguliwa kuwa Rais katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu hajawahi kutiwa hatiani katika Mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali.

Akizunguza na MTANZANIA Jumamosi juu ya hukumu hiyo na hatma ya Zitto kiasiasa katika siku za usoni, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, alisema pamoja na Katiba kutomwekea kizingiti lakini alionyesha shaka hukumu hiyo kutolewa kwa wakati huu ambao nchi inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Lakini pia alionyesha shaka iwapo litatokea jambo lingine na kumweka matatani zaidi Zitto.

“Kifungu cha 67 © na 39 (e) vya Katiba havimzuii kuwania ubunge au urais, lakini tayari hukumu hiyo inamuingiza kwenye ‘Criminal record’ (rekodi ya uhalifu) kitu chochote kitakachotokea baada ya hapo kinaweza kumuathiri lakini tusisahau nchi yetu ina sheria nyingi, unaweza kukuta kuna sheria nyingine ikaja ikaibuka huko mbele inasema tofauti” alitahadharisha Ole Ngurumwa.

Alisema yeye katika uchambuzi wake anaona hukumu hiyo ni pigo pia kwa Zitto kama mwanasiasa ambaye yeye na chama chake kitakwenda kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba.

“Mimi naona kama uminyaji wa demokrasia ni sawa na mtu anayeshiriki mashindano ya mpira halafu ghafla ukamfungia asishiriki mazoezi, kwa mwanasiasa dhana yake ya kwanza ni mdomo, hii hukumu itamnyima haki ya kidemokrasia ya kuzungumza kile anachokitaka kwa uwazi na ukweli kwa sababu hajui watatafsiri vipi.” alisema Ole Ngurumwa.

Mbali na Ole Ngurumwa, Wakili Mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa, makosa yanayomnyima nafasi ya kugombea ni uaminifu na matumizi mabaya ya fedha.

“Katiba iko wazi inasema makosa ya pekee ambayo yanamnyima mtu nafasi ya kugombea nafasi ya umma ni ukosefu wa uaminifu na matumizi mabaya ya fedha japo kuna makosa mengine kama dawa za kulevya sababu lengo la sheria ni kuwalinda wapiga kura dhidi ya mtu ambaye hana uaminifu.

“Sababu ingekuwa hivyo basi Nyerere(Julius Nyerere) asingekuwa Rais wa Tanzania sababu alipatikana na hatia ya uchochezi licha ya kwamba Katiba ya sasa ilikuwa haijaundwa lakini tabia za Katiba hii ni zilezile tu na ile ya mwanzo.

“Hivyo kosa la uchochezi halimzuii mtu kugombea hata siku moja, hivyo kuna makosa mahsusi ambayo yamewekwa hasa yale ambayo yanahusiana na uaminifu ikiwamo rushwa,” alisema Wakili huyo.

Akifafanua zaidi juu ya makosa hayo ambayo yanamnyima mwanya wa mtu kugombea alisema kuwa ni pamoja na kutakatisha fedha ikiwamo pia wizi.

“Kuna makosa mengi karibu saba, ukiacha la kutakatisha fedha kuna kuiba kwa mtumishi wa umma, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu hivyo ukiwa mtumishi wa umma kisha ukavunja hiyo dhamana ya utumishi wa umma basi ni wazi kuwa unakuwa hauruhusiwi,” alisema Wakili huyo.

Kwa upande wake Wakili anayemtetea Zitto katika kesi hiyo, Jebra Kambole alisema kuwa watakata rufaa juu ya uamuzi huo.

“Kifupi tutajadiliana na Mawakili wenzangu, tutakata rufaa Mahakama Kuu, ni uamuzi ambao unatakiwa kukatiwa rufaa sababu hapa kinachoangaliwa ni rekodi ya kufanya jinai tayari, sababu katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 13(6)(a) inasema kuwa kama hujaridhika na maamuzi yoyote unaweza kukata rufaa,” alisema Jebra. 

ZITTO NA URAIS 

Itakumbukwa Desemba 5, mwaka jana Zitto alisema lazima vyama vya upinzani viungane katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, vikiona anatosha kuwania urais atakubali.

Zitto alitoa kauli hiyo wakati wa mahojiano katika kipindi cha Konani cha kituo cha televisheni cha ITV wakati akijibu maswali ya mtazamaji aliyetaka kujua kama ana nia ya kugombea urais kwenye uchaguzi ujao.

Zitto alisema kwa muda mrefu amekuwa na nia ya kuwa Rais wa Tanzania, na kusisitiza kuwa suala hilo si la mtu mmoja bali ni uamuzi wa chama au vyama vya siasa. 

“Iwapo vyama vitaona mimi ndiyo mgombea ninayestahili kupeperusha bendera nitagombea lakini vikiona mtu mwingine ndio anafaa zaidi basi nitamuunga mkono. Lazima tushirikiane kuiondoa CCM madarakani,” alisema Zitto.

Zitto ambaye alisema anaumizwa kuona takribani Watanzania milioni 14.7 wanaishi katika umasikini licha ya wingi wa rasilimali zilizopo alisema akiwa Rais atasimamia zaidi sekta ya kilimo ambayo ndiyo inaajiri watu wengi.

Aliongeza kuwa Serikali haijawahi kutenga hata asilimia tatu ya bajeti yake kwenye sekta ya kilimo, hakuna mradi hata mmoja wa kilimo cha umwagiliaji ambao umezinduliwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles