JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA YA HABARI
DUNIANI kuna mambo, ndivyo unavyoweza kueleza kuhusu simulizi ya kijana huyu mwenye umri wa miaka 25 mkazi wa Buenos Ares nchini Argentina, ambaye anajibadili kuwa katika mwonekano wa kibwengo, malaika na hata shetani.
Mpenzi huyu wa mwonekano wa kubuni, Luis Padron, ametumia zaidi ya pauni 25,000 sawa na zaidi Sh milioni 75 kuufanyia mwili wake upasuaji ili tu afanane na kibwengo halisi.
Uamuzi huo, mbali ya mapenzi yake mwenyewe ya kuwa na shauku na ufahari wa kupata mwonekano huo ulichochewa pia manyanyaso aliyokumbana nayo akiwa mdogo.
Baada ya kukumbwa na mateso ya dhihaka za jinsi alivyo akiwa mdogo huku akiwa hana marafiki, akazama katika dunia ya vibwengo, malaika, shetani na viumbe vingine kwa kutazama filamu na kusoma vitabu kuwahusu.
Akawa amedhamiria kuonekana kama wahusika awapendao katika filamu hizo, akaanza kupausha nywele na ngozi yake kuwa nyeupeee!.
Kwa sasa amejikita katika tiba inayotumia pauni za Uingereza 4,000 sawa na Sh milioni 12 kwa mwezi kuweka krimu, kukausha nywele na kukarabati macho.
Hadi sasa ameshatumia zaidi ya Sh milioni 75 kwa upasuaji ikiwamo kutengeneza midomo, taya, kukarabati pua na kuondoa vinyweleo mwili mzima na operesheni ya kubadili rangi yake ya macho.
Padron katika mwonekano usio wa kawaida, anasema hajali watu wanavyomfikiria na kuwa hatakoma hadi atakapogeuka kuwa kibwengo halisi.
Anapanga kufanya upasuaji kufanya masikio yake yawe ya kuchongoka, kupandikiza nywele ziwe katika umbo la moyo na operesheni ya kurefusha miguu na mikono kumfanya aonekene mwenye urefu wa futi sita na inchi tano.
Kijana huyu ambaya huuza bidhaa za vinyago anasema: “Nataka kuwa kibwengo, ama malaika na au kiumbe chochote cha ajabu cha kubuni, lengo langu ni kuonekana katika hali isiyo ya uanadamu, kiumbe cha peponi.
“Ninataka masikio yangu yawe yenye ncha kali kama kibwengo, taya langu lionekane kali zaidi kama almasi na uso mrefu na macho marefu na kunipatia yenye umbo kama yale ya paka.”
“Nafikiria pia upandikizaji misuli. Kuna upasuaji unaoweza kukufanya uwe mrefu na nitaondoa sehemu ya mbavu zangu nne, ili niweze kutengeneza upya kiuno changu ili kiwe chembamba.”
Aliongeza: 'watu wamekuwa wakiniangalia kwa mshangao tangu nikiwa kijana mdogo, hivyo kwa wanavyonitazama sasa sioni ajabu kwa vile nishazoea. Kwa kuzoea hali hiyo, sasa napenda watu wanitazame kwa kweli na sijali kile wanachofikiria.
'Hata wakati nisipovaa kama kibwengo watu hunitazama. Nina nywele ndefu nyeupe kwa miaka mitano, natumia miwani yenye lensi kubwa na mimi ni mrefu sana.
“Ninatumia vipodozi kutengeneza mwonekano wangu ili uwe wa kimalaika na kuvaa nguo zenye mtindo wa ajabu au za kale.”
“Najiona kama kiumbe wa ulimwengu mwingine, kwa namna ile ile watu wanaobadili jinsia wanavyojisikia katika jinsia mpya. Nahitaji kuwa namna ninavyojisikia kwa ndani, sitarajii watu waelewe ninavyojihisi lakini nataka waheshimu nilivyo.
“Mwonekano wa kubuni unanifanya niwe wa furaha na kwa sababu sina marafiki wengi wakati nilipokuwa mdogo sikuona shida kuzamia katika mwonekano huu.'
Padron aliangukia katika mapenzi na uonekano wa kubuni wakati wa miaka yake ya ujana, akipambana na zomea zomea na udhalilishajui mwingine kutokana na mwonekano na uvaaji wake wa nguo.
Lakini kufikia mwisho wa shule ya juu, alidai mwonekano wake wa ajabu ulimfanya apendwe, kitu ambacho kilichochea zaidi matamanio yake ya kuwa tofauti.
Aliongeza: “nilikuwa nikionewa, dhihakiwa, dhulumiwa nikiwa mtoto na kuondokana na mateso hayo, suluhu nikaona ni kujizamisha na filamu za viumbe vya ajabu kama vile Labyrinth na The NeverEnding pamoja na simulizi nyingine.
“Kwa kipindi fulani vitu vikabadilika, vijana wakubwa wakaanza kunipenda kwa sababu ya mwonekano wangu wa kipekee na hilo lilinitia moyo kuanza kujibadili kwa namna ninavyojisikia kutokea ndani.
'Nilianza kwa kuvaa mavazi na vinyago lakini halikutosha, nilitaka kubadilika kuwa katika mwonekano wa ndoto yangu.”
Katika umri wa miaka 14, nilidhamiria kupitia kisu ili nionekane kama kibwengo na miaka sita baadaye nikapitia upasuaji kwa mara ya kwanza.
Anakumbuka: 'ilikuwa mwanzo uliopelekea kuamua kuwa huo ni mwelekeo sahihi niliouchagua katika maisha yangu. Operesheni haikuwa rahisi kwani maumivu yalitawala lakini mwishowe imekuwa faraja kwa kupiga hatua moja mbele kuelekea ndoto yangu.”
Katika kutimiza ndoto yake ya kuwa kiumbe kisicho cha kawaida katika dunia hii ameendelea kuwa na zaidi ya upandikizaji 40, kuondoa vnyweleo mwili mzima na kupausha ngozi kuondoa mikunjo au alama zozote.
Hali kadhalika, alipitia tiba isiyokubalika katika tasnia ya afya ya kubadili macho kutoka rangi ya kahawia hadi angavu bluu, hali iliyomsababishia maumivu.
Kuhusu hilo anasema lilifanyika bila nusu kaputi na ikabidi atumie dawa ya macho na miwani miyeusi kuyalinda na mwonekano mpya umemfanya aonekane kama mnyonya damu.
“Mwanzoni hata kuangalia nyota angani ilileta shida kwa maumivu lakini baada ya siku tatu hali imerudia kawaida, sifahamu namna yatakavyoathiri uoni wangu siku za usoni,” anasema.