23.3 C
Dar es Salaam
Friday, May 27, 2022

WINGU LA IDD AMIN BADO NI TAMU KIHISTORIA

NA MARKUS MPANGALA,

MASIMULIZI yetu ya leo yanahusiana na wingu linaloizungunga vita vya Kagera, ambavyo Rais wa zamani wa Uganda, Idd Amin alianzisha chokochoko na baadaye akaingia vitani dhidi ya Tanzania.

Ni katika muktadha huo wapo watu waliodiriki kueleza bayana mgawanyiko jeshini, makosa ya rais, wimbi la waasi na harakati mpya za kuidai Uganda yenye mwelekeo wa kidmokrasia ulipomea.

Kitabu chetu wiki hii ni “Cross to the Gun: Idi Amin and the Fall of the Uganda Army.” Kimechapishwa kwa mara ya kwanza (toleo la kwanza) mnamo mwaka 2002. Mwandishi wake ni Kanali Bernard Rwehururu ambaye ambaye alikuwa miongoni mwa wanajeshi wa Uganda walioshiriki vita hiyo.

Zipo jumla ya kurasa 189 katika kitabu hiki na kupewa nambari 9970-411-65-7. Aidha, kimebeba mambo muhimu ya kihistoria kati ya serikali ya Tanzania na ile ya Uganda iliyokuwa ikiongozwa na Iddi Amin.

Mwandishi anaanza kueleza juu ya mapinduzi yaliyotokea nchini Uganda mwaka 1971 kipindi ambacho Rais Milton Obote akiwa ziarani nje ya nchi. Amin alitumia fursa ya ziara hiyo kumpindua Obote ambaye wanatajwa kuwa na msuguano wa kimya kimya kwa muda mrefu.

Kwa wale wapenzi wa vitabu vya historia bila shaka watavutiwa na kitabu hiki. Aina ya masimulizi yake ni kama yale ya kitabu cha jasusi wa zamani hapa nchini Frowin Kageuka ambaye ameandika kitabu cha “Mateka Mpakani” kuelezea masuala ya vita vya Uganda kati ya Idd Amin na Tanzania ya Mwalimu Nyerere.

Kanali Rwehururu ndani ya kitabu chake anabainisha namna ambavyo majeshi ya Uganda yalivyokosa ari kwa muda mrefu kutokana na matatizo ya kutojua kusoma, ukanda, ujinga, mgawanyiko wa ndani ya jeshi, udhalilishaji na uongozi mbaya ambao ulichangia kushindwa vibaya sana kwenye vita hivyo.

Rwehururu anaelezea mauaji ya watu mbalimbali nchini Uganda kulisababisha hali ya sintofahamu, ikiwemo ya Askofu Lumum. Vilevile anaelezea namna Chama cha Ukombozi wa Kipalestina kilivyojiingiza kwenye jeshi la Uganda.

Mwandishi anaelezea juu ya sura mpya za kijeshi zilizoingizwa nchini Uganda kutoka mataifa ya Sudan na Congo, ambapo wengi wao hawakuwa na uwezo wa kusoma na kuandika. Anasema idadi kubwa ya askari hao ndio walioshiriki mapinduzi dhidi ya Obote, licha ya kuwapo baadhi ya askari wa wenyeji.

“Maofisa wachache wa jeshi wenye elimu na mafunzo bora walipewa hadhi na vyeo vya daraja la pili. Wengi walishindwa kutoa mawazo yao juu ya mipango ya kijeshi au ushauri wa tenda za masuala ya kijeshi wakihofia kutoeleweka,”

Rwehururu, ambaye alijiunga na Jeshi la Uganda mwaka 1965 anasema miongoni mwa mambo yaliyoshangaza ni kuwatimua watu wenye asili ya Asia ambao walikuwa raia wa nchi hiyo.

Ikumbukwe kuwa maelfu ya watu wenye asili ya Asia waliofukuzwa Uganda walikimbilia nchini Uingereza. Ndiyo kusema ndani ya taifa hilo hakukuwa na uongozi wa kueleweka  zaidi ya wananchi wa Uganda kushuhudia vituko na tabia binafsi za Iddi Amin pamoja na askari waliokuwa wakimtii.

Anasema kulikuwa na mambo ya ajabu kama yale ya kuwateua askari au watu waliomtii huku wakiwa hawajui kusoma wala kuandika kuongoza kwenye taasisi za kibiashara za umma.

Aidha, anasema kulikuwa uhalifu ndani ya idara ya usalama ya nchi hiyo (State Research Bureau, SRB), hivyo hata mapinduzi yalipotokea kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakimtii Idd Amin.

Anasema kupinduliwa Obote kulisababisha uhusiano mbaya kati ya Tanzania na Uganda. Nchi hizi zilituhumiana kwa muda mrefu, huku Obote akipewa hifadhi Tanzania hali iliyomuudhi Idd Amin.

Vilevile kunaelezwa kulikuwa na wakati mgumu wa abiria waliokuwa wakijaribu kusafiri kati ya Tanzania na Uganda hali ambayo ilizidisha msuguano na kuchochea zaidi vita vya Kagera.

Mwandishi anasema kuibuka vikundi vya FONASA (Front for National Salvation) vya Yoweri Museveni na Kikosi Maalumu la Oyite Ojok kuliamsha mapambano dhidi ya Idd Amin, mbaya zaidi kundi la Museven lilitokea upande wa Tanzania.

Anasema hali hiyo ilichangia kuongeza msuguano, ambao mwaka 1978 hali ilikuwa mbaya zaidi mashushushu wa Tanzania waliokuwa kwenye Kituo cha Shule ya Ufundi ya Masaka (Masaka Technical School) alikamatwa na askari wa Amin (hapa ndipo tunakumbuka masimulizi ya kitabu cha Mateka Mpakani juu ya kutekwa kwa kachero Frowin Kageuka). Kwamba ulikuwa ujasusi dhidi ya ujasusi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,437FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles