Na ELIYA MBONEA-ARUSHA
ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, Dk. Stanley Hotay, amewataka wafugaji wa Kimaasai wilayani Ngorongoro, Mkoa wa Arusha, kuhakikisha wanalitunza Bonde la Ngorongoro ili lizidi kuwaletea maendeleo wao na Watanzania.
Askofu Dk. Hotay alitoa kauli hiyo juzi kijijini Kakesyo, Tarafa ya Ngorogoro, wakati wa uzinduzi wa Shule ya Msingi Enyorata Ereko iliyojengwa na Mwinjilisti Jane Kim (Mama Maasai), raia wa Marekani mwenye asili ya Korea anayefanya kazi ya uinjilisti na kanisa hilo.
Mama Maasai alitembelea eneo hilo akiwa mtalii aliyekuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali na kabla ya kurudi kwao, aliahidi kurudi Tanzania kwa ajili ya kufanya kazi ya Mungu kwenye eneo hilo ikiwamo ujenzi wa makanisa na shule.
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyohudhuriwa na mgeni rasmi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Jimbo hilo, William ole Nasha, Dk. Hotay alisema wafugaji wanapaswa kutambua kuwa, wanaishi eneo muhimu linaloileta dunia nchini Tanzania.
Alisema kwamba, kutokana na umuhimu wa Bonde la Ngorongoro, wafugaji wanaoendesha shughuli zao wanapaswa kulitunza bonde hilo kwa kupunguza mifugo yao na kuwekeza katika maeneo mengine yatakayowawezesha kuendelea kujiingizia kipato zaidi.
“Mmepewa eneo muhimu linaloileta dunia nchini Tanzania. Kama mngeamua kukata miti, kuharibu mazingira na kuua wanyamapori, basi haya mataifa tunayoyaona yakija kutembelea Bonde la Ngorongoro yasingeweza kuja.
“Wafugaji mnaofuga ng’ombe wengi nawaomba mtumie ng’ombe wenu kwa faida kuliko wafe kwa kukosa malisho.
“Wauzeni wakiwa katika soko la Shilingi milioni 1 au zaidi, wekezeni kwingine huku mkiendelea kubakia na mifugo michache mnayoweza kuitunza,” alisema Askofu Dk. Hotay.