27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu Mtetemela: Watanzania msikate tamaa

dk-donald-mtetemelaNa Mwandishi Wetu

ASKOFU mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Donald Mtetemela, amewataka Watanzania kuacha kukata tamaa pindi wanapokutana na vikwazo wakati wa kutekeleza ndoto zao za maisha.

Askofu Mtetemela aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mradi wa huduma ya mikopo inayohusisha vifaa inayojulikana kwa jina la Karadha na inayotekelezwa na Shirika la Mama Bahati Foundation la mjini Iringa, ambapo askofu huyo alisema Watanzania  wengi wamekuwa wakikwama kufikia ndoto zao kutokana na changamoto mbalimbali.

Mtetemela aliwataka Watanzania kuacha kuruhusu changamoto zinazopatikana katika maisha na kushindwa  kufikia ndoto walizojiwekea na badala yake akawataka kutafuta mbinu mbadala za kukabiliana na changamoto hizo.

Katia hafla hiyo, Askofu Mtetemela aliwakabidhi wanawake watatu pump za kuendeshea kilimo cha umwagiliaji kama sehemu ya kuanza kutolewa kwa mkopo huo wa vifaa wenye lengo la kusaidia wakinamama kukabiliana na changamoto za umasikini.

Alisema pamoja na shirika hilo la Bahati Foundation kutoa mikopo ya vifaa hivyo kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali likiwamo Shirika la Swiss contact lenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam, jambo la muhimu kwa wateja wanaokopesha vifaa hivyo kuvitumia ili kuweza kuzaa matunda.

“Vifaa hivyo mlivyokabidhiwa leo vitakuwa na thamani kubwa, ikiwa ninyi mtakwenda kuvitimia kwa shughuli za maendeleo, lakini inawezekana visiwe na tija kwenu endapo mtafika na kuviweka ndani na msivitumie,” alisema Askofu Mtetemela na kuongeza:

“Jambo jingine linaloweza kuwasaidia kufikia malengo mliyojiwekea ni kuwa waaminifu kwa wale mnaokwenda kufanya nao kazi, lakini pia hata kwa hawa waliowapatia mikopo yenu, ikiwa ni pamoja na kurejesha marejesho yenu kwa wakati,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Mama Bahati Foudnation la Mjini Iringa, Japhet Makau, alisema tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 2007 hadi sasa, limefanikiwa kutoa mikopo kwa wateja zaidi ya 16,000 na kwamba kwa sasa limetenga Sh milioni 100 kwa ajili ya kutekeleza mradi mpya wa mkopo wa vifaa (Karadha).

Alitaja vifaa wanavyotarajia kutoa katika kipindi cha kwanza cha majaribio kinachoanzia sasa hadi julai 2017, kuwa ni pampu za maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, mzinga ya nyuki, mashine za kupasulia mbao na vyereheni.

“Vifaa hivyo tunavyoanza navyo ni matokeo ya hitaji la weteja wetu ambao kabla ya kufanya uzinduzi wa mradi huo, tulikuwa na jukumu la kuwapatia semina ya namna ya kutumia fursa hii ya mkopo, ikiwamo ya kuvielewa vifaa na namna ya kuvitumia,” alisema Makau.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa shirika hilo waliopata mkopo wa pampu za umwagiliaji ya kuendesha kilimo cha umwagiliaji, Zamda Salum, alilishukuru shirika hilo kwa kutoa mkopo huo na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia kuongeza pato katika familia zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles