25.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 18, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu Mathias Isuja afariki dunia

askofuNA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

ALIYEKUWA Askofu wa Jimbo Kuu la Dodoma la Kanisa Katoliki, Mathias Isuja (87)  amefariki dunia  katika Hospitali  ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar Itigi mkoani  Singida.

Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Dodoma, Padre Chesco Msaga, alisema askofu huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia jana.

Alisema  alikuwa akisumbuliwa na saratani ya tumbo.

“Tumepata  msiba Jimbo Kuu la Dodoma kutokana na kifo cha Mhashamu Askofu mstaafu Mathias Isuja. Kifo kimetokea usiku wa kuamkia leo (jana) katika Hospitali ya Rufaa   Itigi,”alisema Padre Chesco.

Alisema mazishi yatafanyika Jumatano ijayo   jimboni hapo na tayari mwili wa marehemu umekwisha   kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

“Tunaomba waumini waendelee kushikamana katika kipindi hiki kigumu cha majonzi cha kuondokewa na Askofu wetu,”alisema.

 

Alisema mwaka jana Askofu Isuja alikwenda  India kabla ya kurejea Tanzania na kuendelea na matibabu kutokana na ugonjwa huo wa saratani ya tumbo.

Isuja alizaliwa Agosti 14 mwaka 1929, Haubi wilayani  Kondoa.

Alianza masomo  yake ya ukasisi   Desemba 24 mwaka 1960 na kupewa Daraja Takatifu la Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Dodoma.

Juni 26 mwaka 1972 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Dodoma na kuwekwa wakfu   Septemba 17 mwaka 1972 kabla ya kustaafu   Januari 15 mwaka 2005.

Wakati huohuo, Rais Dk  John   Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Askofu Tanzania (TEC) Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa kutokana na  kifo cha Askofu mstaafu   Mathias Issuja.

Katika salamu hizo Rais Magufuli amesema Askofu mstaafu Mathias Issuja alikuwa mzalendo wa kweli, kipenzi cha watu, aliyefanya kazi kubwa ya kuwajenga watu katika roho na  mwili, na kamwe mchango wake katika maendeleo ya elimu, afya na malezi ya watoto yatima hautasahaulika.

“Nimepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Baba Askofu Mathias Issuja. Kazi kubwa aliyoifanya duniani kuwahudumia watu kiroho na kimwili ni vigumu kuipima, nitamkumbuka daima,”  alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles