27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga, Azam FC zaipumulia Simba

32NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jana walizidi kuwapa presha mahasimu wao Simba baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui FC, huku Azam ikiiangamiza Mtibwa Sugar mkoani Morogoro.

Kwa matokeo ya jana, Yanga iliyoikaribisha Mwadui katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ilifikisha pointi 56 na kuzidi kuipumulia Simba huku Azam ikifikisha pointi 55 kutokana na ushindi wa bao 1-0 waliopata dhidi ya Mtibwa katika Uwanja wa Manungu, Morogoro.

Vinara Simba wanaoongoza kwa kujikusanyia pointi 57, wanazidi kupata mchecheto kutokana na mahasimu wao Yanga kubakiwa na mchezo mmoja wa kiporo wakati Azam wakiwa tayari wamemaliza baada ya kucheza mechi 24 sawa na Wekundu hao wa Msimbazi.

Yanga wameendelea kutetea nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakitofautiana pointi moja na vinara Simba, wakati Azam imebaki nafasi ya tatu kutokana na pointi 55 walizojikusanyia huku wakifuatiwa na Mtibwa wenye pointi 43.

Katika mchezo wa jana, wenyeji Yanga ndio walikuwa wa kwanza kutikisa nyavu za wapinzani wao dakika ya tatu kwa bao safi lililofungwa na kiungo, Simon Msuva, aliyeunganisha krosi iliyochongwa na mlinzi, Oscar Joshua.

Bao hilo liliwazindua Mwadui ambao walikuja juu na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 13 kupitia kwa Kelvin Sabati aliyewazidi maarifa mabeki wa Yanga na kupiga shuti lililodakwa na kipa Deogratius Munishi na kumponyoka na kupata urahisi wa kufunga.

Yanga waliendeleza mashambulizi langoni kwa Mwadui ambapo dakika ya 24 mshambuliaji, Donald Ngoma, alipata nafasi ya wazi kutokana na pasi ya Amissi Tambwe lakini alishindwa kuitumia baada ya kupiga shuti lililotoka nje.

Dakika ya 70 mwamuzi Selemani Kinugani kutoka Morogoro alimwonyesha kadi ya pili ya njano na kumtoa nje kwa kadi nyekundu mchezaji wa Mwadui, Iddy Mobby, baada ya kumfanyia madhambi Ngoma.

Bao la pili lililoipa ushindi muhimu Yanga lilifungwa dakika ya 86 na kiungo, Haruna Niyonzima, kwa shuti kali baada ya kuunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na Ngoma.

Kwa upande wa Azam FC, bao pekee la ushindi liliwekwa wavuni na mshambuliaji, John Bocco, kwa mkwaju wa penalti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles