30.1 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu Gwajima awindwa

Josephat Gwajima
Josephat Gwajima

* Polisi wazingira nyumba yake kwa saa kadhaa

* Ni baada ya kurusha kombora kwa Kikwete

VERONICA ROMWALD NA ASIFIWE GEORGE, DAR ES SALAAM

WATU sita wanaodhaniwa kuwa askari wa Jeshi la Polisi, wamevamia na kuizingira nyumba ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima nchini, Josephat Gwajima.

Tukio hilo linadaiwa kutokea jana mchana katika makazi ya askofu huyo yaliyoko eneo la Salasala, Dar es Salaam.

Inadaiwa watu hao walifika nyumbani kwa askofu huyo wakiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser, na kwenda kugonga geti ili wafunguliwe waingie ndani.

Picha mbalimbali zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii jana, ziliwaonyesha watu hao wakiwa wameizingira nyumba hiyo, huku wakiwa wamebeba bunduki zao vifuani.

Kitendo cha kuzingirwa nyumba ya askofu huyo aliyejibatiza jina la ‘Mr Tanzania’, kilizusha hofu miongoni mwa waumini wa kanisa lake na kuibua mijadala kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Kupitia ukurasa wa mtandao wa Facebook wa kanisa hilo, Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano, David Mgongolwa, alililazimika kulitolea ufafanuzi tukio hilo.

Mgongolwa aliandika: “Kuhusu kuzingirwa kwa nyumba ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Duniani, Dk. Josephat Gwajima mchana huu na watu wasiojulikana.

“Viongozi wa Juu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Duniani pamoja na mwanasheria wa kanisa wanafuatilia kwa karibu na tutatoa taarifa kamili hapo baadaye. Tunaomba watu wote tuwe watulivu.”

Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA lilimtafuta Askofu Gwajima ili kupata sababu za kutafutwa na polisi, lakini simu yake ya kiganjani haikuwa hewani.

Msaidizi wa askofu huyo, Jerald Budodi, alipotafutwa alisema hayupo Dar es Salaam.

“Sipo Dar es Salaam leo (jana) nipo Mwanga (Kilimanjaro), ni vyema umtafute Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi maana yeye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya hiyo, pengine anaweza kujua,” alisema.

MTANZANIA lilimtafuta Mkuu wa Wilaya hiyo, lakini hata hivyo hakupokea simu badala yake alituma ujumbe mfupi wa maandishi kuwa alikuwa kwenye kikao.

Alipojulishwa juu ya tukio hilo kupitia ujumbe mfupi wa maandishi, hakuujibu hadi tunakwenda mitamboni.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime atoe ufafanuzi juu ya tukio hilo, alikana kuwa watu hao walioizingira nyumba ya Askofu Gwajima si askari wake.

“Nyie waandishi bwana mnanisumbua… wengine wamenipigia wanasema ni watu wasiojulikana, wewe unaniambia ni askari, sasa hapa nielewe nini. Watu hao si askari wangu… lakini inawezekana wameenda kumhoji,” alisema.

Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Siro, alipotafutwa kuelezea kuhusu tukio hilo alisema yupo kwenye kikao.

 MAHUBIRI YAKE

Mara kwa mara Askofu Gwajima amekuwa akisikika katika mahubiri yake mbalimbali akikikosoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kilichopo madarakani.

Aprili 17, mwaka huu akihubiri kanisani kwake, aliuchambua utendaji kazi wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli na kusema baadhi ya wanachama wa CCM wanamchukia na kumuona kuwa ni sawa na kirusi.

“Wakati Magufuli alipotangaza kugombea, wengi walijua naye ataifuata mifumo hiyo, lakini amekuwa kinyume chao ndiyo maana wanamuona ni sawa na kirusi aliyekwenda kuharibu mipango yao…  Na ndiyo maana leo anapowabana wala rushwa, wakwepa kodi na wauza dawa za kulevya wanampinga, wanamuona hafai, mimi nasema acha aendelee kuwakanyaga hadi dunia yote ijue,” alisema.

Lakini kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana uliompa ushindi Dk. Magufuli na kuwa rais, askofu huyo alisikika akiiponda CCM na kuwataka Watanzania wamchague mgombea aliyesimamishwa kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa.

Juni 11, mwaka huu alisisitiza: “Moyo wangu unasema Tanzania mpya inakuja… kwa sababu anayeileta ni Mungu kupitia watu, kwa Mungu huwa mzoga unatoa asali na mimi huwa nasema wazi hata wakati wa uchaguzi nilikuwa simpendi Magufuli wale watambaji sikieni, nilikuwa simpendi, Magufuli yeye binafsi sikuwa na tabu naye, lakini nilikuwa na tabu na ile kitu inaitwa CCM.

“Wala sikutegemea kwamba atakuwa rais na nilikuwa nasema Mungu aje mtu mpya asiyetoka CCM ndiyo maana hukuniona mahali popote nimesema hiyo kitu nzuri… mimi nasemaga kweli, naona watu wameanza kukodoa macho… kodoa vizuri, mimi sikuwa naipenda CCM, siwasemei nyinyi, nilikuwa napenda iondoke kabisa, kwanini nilisema hivyo… sababu zenyewe ni zile alizozisema Magufuli alipoingia madarakani.”

Aliongeza: “Kwa taarifa yako tulikuwa tunamjua ni mchapakazi, lakini akiingia madarakani hili dudu hili, rafiki yangu Mbowe alisema kwamba hata malaika akishuka mbinguni ndani ya jitu hili anakuwa ibilisi. Malaika Gabriel ukimshusha pale ndani ya sekunde chache anageuka kuwa ibilisi, mtanisamehe watu mnaopenda hiyo kitu, lakini mimi ni mtumishi wa bwana huwa nasema ili watu wapone, tulikuwa tunatamani hii kitu iondoke, lakini imekuja tena.

“Bahati nzuri alichaguliwa Magufuli, ni mkali na anawashughulikia wale wale aliowachagua, hana simile, yaani anapiga tu, nikasema wiki iliyopita kama Magufuli anawachakaza kweli anatakiwa ajue wale wengine anaowachakaza waliagizwa na yule kwa sababu alikuwa anawapa maelekezo. Hatukutegemea, ameanza kufanya kazi ambayo inatupa matumaini.”

Askofu huyo alisema ameyasema hayo kwani Rais Magufuli ameingia madarakani siku 60 za mwanzoni aligundua ‘flow meter’ ilikuwa haifanyi kazi.

“Ina maana mafuta miaka mitano yaliingia nchini bila kulipiwa ushuru, aliyekuwa kwenye nafasi hiyo kwa miaka 10 hakuona, jibu likaja alikuwa kimya, inatafasiri yake ya kwanza ‘am confortable’, pili nimekuruhusu na tatu usiguse hapo ni mali yangu.

“Aliona makontena zaidi ya 2,000 yametoroka bila kulipiwa ushuru na yaliletwa hajawa rais, ilikuwaje polisi wapo na usalama wa taifa wapo, hawakuyakamata kwa sababu ni ya yule mzee.

“Amekamata watumishi hewa, yule aliyetoka alikuwa hawaoni, CCM kwa utaratibu wao Juni wanatakiwa wamkabidhi unyekiti ili awe na kofia mbili ya urais na uenyekiti, lakini nimepata taarifa zangu za kiufufuo kwamba wale waliokuwa wameleta makontena bila kulipia ushuru, wafanyakazi hewa, walioharibu ‘flow meter’ wakisimamiwa na yule babu yao, wanazunguka nchi nzima ili walete hoja kwamba Magufuli asipewe uenyekiti wa chama maana anatumbua sana kila mahali,” alisema.

Askofu huyo alimshauri Magufuli kwamba kwa kuwa CCM wanataka kumnyima uenyekiti wa chama, apeleke muswada bungeni ili aondoe kinga na rais ashtakiwe kwa makosa aliyoyafanya akiwa madarakani.

“Ikiondolewa kinga ndiyo tutajua mwendo kasi ni wa nani, UDA alinunua nani, NIDA ilikuwa ya nani, meli iliyokamatwa na pembe za ndovu kule China ilikuwa ya nani, dawa za kulevya za nani, waachie uenyekiti wao ila ondoa kinga kisha mahakama ya mafisadi ianze nao,” alisema katika mahubiri yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles