22.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaitengea IPTL bilioni 100/-

iptl

Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

IKIWA bado Watanzania hawajasahau mzimu wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), ambao uling’oa vigogo katika sakata la fedha za akaunti ya Tegeta Escrow, sasa Serikali imeitengea Sh bilioni 100 kwa ajili ya kubadili mitambo yake ili iweze kutumia gesi asilia.

Hatua ya kampuni hiyo kutengewa fedha na Serikali inakwenda kinyume na maazimio ya Bunge likiwemo la kutaka kutaifishwa kwa mitambo hiyo ambayo kwa sasa inatumia mafuta mazito, ili iwe mali ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Hayo yameibuliwa jana na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), aliyeweka taarifa hiyo kwenye ukurasa wake wa Facebook, akionyesha kushangazwa na hatua ya Serikali kutenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuipa kampuni hiyo ambayo si mali yake.

Katika taarifa yake hiyo ambayo iliibua mjadala mzito, Zitto  alihoji Serikali inayopambana na ufisadi inawezaje kutoa fedha za umma kuipa kampuni aliyoiita ya kifisadi.

Kampuni ya IPTL ilikumbwa na kashfa kubwa ya uchotwaji wa Sh bilioni 321 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na kusababisha mawaziri na viongozi wengine wa Serikali kujiuzulu.

Kutokana na kashfa hiyo, Bunge lilipitisha maazimio manane huku likiitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine kuwachukulia hatua stahiki mmiliki wa IPTL, Harbinder Singh Seth na wengine.

Pia Bunge liliazimia Serikali kuangalia uwezekano wa kuichukua mitambo ya kampuni hiyo na kuimilikisha kwa Tanesco kwa mujibu wa sheria za nchi.

Bunge liliazimia kupitiwa kwa mikataba ya umeme na Serikali kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Takukuru kwa ajili ya kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa.

Katika azimio la tano, Bunge liliimtaka rais kuunda tume ya kijaji ya uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji waliotuhumiwa.

Azimio la sita, lilitaka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank na benki nyingine yoyote itakayogundulika kutokana na uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.

Azimio la saba, ilitaka mawaziri, mwanasheria mkuu wa Serikali na katibu mkuu na Bodi ya Tanesco kuwajibishwa kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi huo, jambo ambalo lilifanyika.

Katika azimio la nane na la mwisho, Bunge liliitaka kamati husika za kudumu za Bunge kuchukua hatua za haraka.

Katika taarifa hiyo ya jana, Zitto ambaye pia ni kiongozi wa ACT-Wazalendo, alisema amesoma nyaraka za bajeti na kuona kuwa Serikali imepanga kiasi cha Sh bilioni 100 kwa ajili ya kubadililisha mtambo huo kuwa wa gesi asilia.

“Nasoma nyaraka za bajeti naona Serikali imepanga fedha kubadilisha mtambo wa IPTL kwenda kuwa wa gesi. IPTL ni kampuni binafsi ambayo inamilikiwa kiutapeli na Kampuni ya PAP kufuatia wizi wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu. Serikali inayopambana na ufisadi inawezaje kutoa fedha za umma kuwapa kampuni ya kifisadi?

“Hawa PAP (Kampuni ya Pan Africa Power) walikuja nchini na briefcase, wakachota fedha BoT wakahonga maofisa wa Serikali, wabunge, majaji, mawaziri, maofisa usalama. Wakapewa mtambo bure. Wanalipwa kila mwezi mabilioni ya ‘capacity charges’,” alisema.

Kutokana na hilo, alihoji ni vipi sasa wanaendelea kufadhiliwa na Serikali kugeuza mtambo wao kuwa wa gesi asilia.

Alimtaka Rais Dk. John Magufuli kulitazama suala hilo la IPTL na si kulalamika kila siku kuwa nchi imekuwa shamba la bibi.

“Kweli Serikali inatenga fedha kuifadhili kampuni hii? Maazimio ya Bunge yanasiginwa namna hii?… Huu mradi wa kitapeli wa IPTL una nguvu ya nani,” alihoji.

 KAULI YA PROF. MUHONGO

Alipoulizwa kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu hilo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alimtaka mwandishi wa gazeti hili awatafute Tanesco ili waweze kutoa ufafanuzi.

Hata hivyo, alisema tayari alikwishaliambia Bunge kuwa mikataba yote ya makampuni ya umeme ni mibaya na kwamba ni wajibu wao kuirekebisha.

“Wasiliana na Tanesco kupata ukweli wa mikataba yao yote… nililiambia Bunge kwamba mikataba yote ni mibaya, ni wajibu wetu kuirekebisha. Haupo mkataba mzuri… isemeni yote.

“Watu wawe wakweli wajadili mikataba yote na si mmoja tu… yote ni mibaya,” alisema Profesa Muhongo.

Pamoja na hilo, alisema leo (jana) Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden amemthibitishia kuwepo fedha za miradi ya wizara yake tangu mwaka 2014.

“Miradi ya nishati kuendelea kupata ufadhili wa Sweden. Leo Alhamisi Ministry of Foreign Affairs wa Sweden amenithibitishia kuwepo kwa fedha za miradi tangu mwaka 2014 hadi leo hii, jumla ya dola milioni 51 zimeshatolewa… kuanzia sasa na kuendelea fedha za ziada dola milioni 190,” alisema.

Gazeti hili lilipomtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba simu yake haikupatikana hadi linakwenda mtamboni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles