30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu aonya ubaguzi wa dini

Nabii Paul Bendera
Nabii Paul Bendera

NA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

KIONGOZI wa makanisa ya Ufunuo nchini, Askofu Paul Bendera, amewashauri Watanzania kuacha kubaguana kwa misingi ya dini kwani ubaguzi husababisha dhambi nyingi na kuzaa migogoro isiyoisha.

Akizungumza Dar es Salaam jana, alisema watu wanapobaguana kwa misingi ya dini huwa hawawezi kuaminiana wala kufanya shughuli  zozote za maendeleo.

“Yanayotokea katika nchi za wenzetu leo hii yawe somo katika nchi yetu kwa sababu vitendo hivi vimekuwa vikiwatesa sana watu kisiasa na kiuchumi, hali hii ni chanzo cha amani kutoweka.

“Sisi viongozi wa dini pia ni vizuri tushirikiane kwa sababu kama hatutakaa pamoja, tutakuwa chanzo cha migogoro ya udini katika Taifa letu.

“Watu wanaweza wakalalamika kwanini umemkaribisha sheikh kanisani au mchungaji kukaribishwa msikitini, huo tayari ni mgogoro tusiogopane tunatakiwa kuwa na umoja na kushirikiana,” alisema Askofu Bendera.

Pia aliwataka viongozi wa dini kuacha kutumika vibaya na kuwapandikizia chuki waumini kwani hali hiyo itasababisha mmomonyoko wa maadili na kuwagawa waumini.

Alisema inapotokea migogoro ni wazi kuwa watu watashindwa kushirikiana katika jambo lolote na kushauri wajijengee utaratibu wa kuvumiliana katika changamoto zilizopo.

Kiongozi huyo alisema pia mashambulizi katika makanisa yanatakiwa kukomeshwa mara yanapoibuka ili kuepusha hasira na malumbano baina ya pande mbili.

Kwa muda mrefu sasa dhana ya udini na ukabila imekuwa ni tatizo sugu linalozitesa nchi nyingi na kusababisha kuingia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles