Wafanyakazi Vodacom wapanda Mlima Kilimanjaro

Mkuu wa Vodacom Kanda ya Kaskazini,Henry Tsamburakis akimsaidia mmoja wa wageni hao kubadili lugha ya kiswahili katika simu yake kwenda ya Kiingereza.
Mkuu wa Vodacom Kanda ya Kaskazini,Henry Tsamburakis akimsaidia mmoja wa wageni hao kubadili lugha ya kiswahili katika simu yake kwenda ya Kiingereza.
Mkuu wa Vodacom Kanda ya Kaskazini,Henry Tsamburakis akimsaidia mmoja wa wageni hao kubadili lugha ya kiswahili katika simu yake kwenda ya Kiingereza.

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

WAFANYAKAZI  36 kutoka kampuni mbalimbali nchini  Afrika Kusini  ikiwemo Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom, wameshiriki mpango wa kupanda Mlima Kilimanjaro  kuchangia jamii ujulikanao kama TREK4MANDELA na fedha zitakazopatikana zitasaidia kuwapatia watoto wa kike elimu ya afya ya uzazi na taulo za kinga wakati wa hedhi.

Mpango huu wa TREK4MANDELA umekuwa ukienda sambamba na makampuni ya Afrika Kusini kushiriki katika shughuli za  kijamii kila mwaka kama sehemu ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mwasisi wa Taifa la Afrika ya Kusini, Hayati Nelson Mandela na kwa mara ya pili kampuni ya Vodacom Tanzania imedhamini msafara wa wapanda mlima hao kwa kuwapatia mawasiliano.

Akizungumza wakati wa kuwakabidhi vifaa vya mawasiliano, Mkuu wa Vodacom kanda ya Kaskazini, Henry Tsamburakis,  alisema kampuni ya Vodacom Tanzania imetoa vifaa vya mawasiliano ili kuwezesha msafara wa wapanda mlima hao na kuhakikisha hawapati tatizo la mawasiliano  na marafiki, ndugu na familia zao ikiwemo  kutuma picha za matukio katika safari hiyo ya kupanda  mlimani.

“Vodacom Tanzania tunajivunia kwa kuwadhamini watalii na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni yetu kutoka Afrika ya Kusini kwa mwaka wa pili mfululizo kwa kudhamini Mfuko wa Mandela ambapo kila mwaka watalii huja nchini mwetu Julai kupanda mlima  Kilimanjaro wakiwa na lengo la kuchangisha pesa kwa ajili ya  kusaidia watoto wa kike,” alisema Tzamburakis.

Alisema Vodacom imetoa vifaa maalumu vya mawasiliano (Routers) sita  zikiwa zimeunganishwa katika mtandao wa kasi  wa 4G huku zikiwa zimewekewa vifurushi vya GB 10 watakazoweza kutumia kwa muda wote watakapokuwa katika zoezi la kupanda mlima Kilimanajaro .

Akizungumza kwa niaba ya wenzake kwenye msafara huo, Gerry Elsdon,  ameshukuru Vodacom kwa kuwafadhili mawasiliano ambayo yatarahisisha safari yao ya kupanda Mlima hadi kileleni

“Kwa niaba ya wenzangu tunashukuru Vodacom Tanzania kwa kutupatia mawasiliano ya kuendelea kutuunganisha na wenzetu popote pale walipo,” alisema Elsdon.

Kwa upande wake, Mratibu wa safari hiyo ,Richard Mabaso ambaye ni mwanzilishi wa taasisi ya Caring4Girls,   alisema lengo la safari hiyo ni kuendelea kuchangisha fedha kwa ajili ya kununua Taulo za kike kwa watoto wa kike wasio na uwezo ili kujihifadhi na kuendelea na  shughuli zao za kila siku kama kawaida wakiwa salama na wakijiamini.

“Tunatambua changamoto zinazowakabili watoto wa kike hasa wale walioko shuleni pindi wanapoingia katika siku zao, kupitia Mfuko wa Mandela tumeendelea kuchangisha pesa kwa ajili ya kuwasaidia angalau kupata taulo ili waweze kuendelea na masomo bila ya kuwa na kikwazo,” alisema Mabaso.

Jitihada za kupambana na changamoto za vipindi vya hedhi pia zimekuwa zikifanywa na taasisi mbalimbali hapa nchini ikiwa ni pamoja na Vodacom Tanzania Foundation ambayo imekuwa ikifadhili mradi wa Girl Power unaoendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la T-MARC ambao umewezesha kupunguza utoro kwa wasichana waliokuwa wanakosa  masomo kutokana na kukosa  vifaa vya kuwakinga wakati wa hedhi na kutokuwapo na miundombinu rafiki shuleni.

Mpango huo unaratibiwa kupitia taasisi ya Imbumba Foundation inayoendesha mradi wa wasichana ujulikanao kama Caring4Girls nchini humo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here