23.5 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

ASILIMIA 43 YA WATOTO WACHANGA WAKUTWA NA HOMA YA ZIKA

zika-confirmed-in-lehigh-university-student-f3a7f01613e578a0

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

ASILIMIA 43.8 ya watoto wachanga 80 kati ya watu 533 ambao walichukuliwa sampuli na kupimwa, wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya homa ya Zika, imeelezwa.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Bugando hivi karibuni, umethibitishwa kuwapo tatizo hilo.

Mkurugenzi wa NIMR, Dk. Mwele Malecela, alitoa kauli hiyo mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya taasisi hiyo kwa mwaka 2016.

Alisema utafiti huo ulilenga kuainisha uwapo wa maambukizi ya virusi vya Zika katika jamii ya Watanzania  na kuangalia athari ya maambukizi katika kusababisha watoto wanaozaliwa na ulemavu.

“Tulipima sampuli za damu kutoka kwa watu 533. Kati yao, watoto wachanga 80 walizaliwa na ulemavu wa viungo mbalimbali. Kati ya waliopimwa asilimia 15.6 waligundulika wameambukizwa virusi vya Zika.

“Kati ya wale watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu, asilimia 43.8 walikuwa wameambukizwa virusi vya Zika. Utafiti unaendelea kujua ukubwa wa tatizo hili,” alisema.

Alisema kutokana na mlipuko mkubwa wa ugonjwa wa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi miaka michache iliyopita, NIMR kwa kushirikiana na Kampuni ya dawa ya Janssen & Jansen, ilifanya majaribio ya awali ya chanjo ya Ebola (Ebovac) katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria.

“Tulihusisha watu 25 na wote walimaliza dozi ya chanjo kama inavyotakia. Matokeo yameonyesha chanjo hii (Ebovac) ni salama kwa binadamu na ina uwezo wa kujenga kinga dhidi ya virusi vya Ebola, tunaendelea na ufuatiliaji kutathmini athari za muda mrefu za chanjo hiyo,” alisema.

Mbali na ugonjwa huo, Dk. Malecela alisema taasisi yake ilifanya pia utafiti kwa kundi la vijana waoendesha pikipiki maarufu bodaboda Agosti, mwaka huu kwa lengo la kutathmini viashiria vya maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) katika Mkoa wa Dar es Salaam.

“Utafiti huo umeonyesha kiwango cha maambukizi ya VVU kwa waendesha bodaboda ni kidogo kwa asilimia 2.5, vijana wengi wameonekana kuwa na tabia hatarishi zinazoweza kuwafanya wapate VVU.

“Tabia hizo ni kama vile kuwa na wapenzi wengi, baadhi kutotumia kondomu na kutofuatilia ili kupata huduma ya ushauri nasaha na vipimo,” alisema.

Dk. Malecela alisema taasisi inapendekeza kufanyika utafiti huo katika maeneo mengine kwa kujumuisha makundi mengine ambayo yako hatarini kuambukizwa.

Alisema pia wameanza majaribio ya chanjo chini ya mkakati mpya kupitia mradi wa P5.

“Majaribio haya yanafanyika, Botswana, Zimbabwe, Msumbiji, Zambia, Malawi, na Kenya. Chini ya mpango huu, washiriki wenye umri kati ya miaka 15-50, wasio na maambukizi ya VVU na magonjwa sugu wanashiriki katika awamu mbalimbali za utafiti.

“Tanzania inashiriki majaribio haya kwa kushirikiana na washirika wake, Mpango wa Utafiti wa Jeshi la Marekani na Mtandao wa Tafiti za Ukimwi Duniani. Mpaka sasa taasisi imesajili washiriki 17 kati ya 28 wanaotegemea kusajiliwa kwenye mojawapo ya tafiti hizi za chanjo,” alisema.

Alisema NIMR imeanza kufanya utafiti wa kufuatilia usugu katika dawa za kurefusha maisha (ARV) kwa watu wanaotumia.

“Tulifanya pia tafiti za VVU na Ukimwi na kutathmini utekelezaji wa mpango wa kupima watoto wachanga, tumebaini bado kuna changamoto kadhaa.

“Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa vipimo vya zamani na vipya vyote bado vina umuhimi katika utambuizi wa maambukizi ya KK kutegemeana na aina mbalimbali za ugonjwa huo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles